Wakenya wajiandaa kutafuna minofu ya ziara ya Macron
NA ANITA CHEPKOECH
ZIARA ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron nchini huenda ikailetea Kenya manufaa ya Sh6 bilioni na nafasi 50,000 za ajira kutoka kwa serikali ya Ufaransa.
Fedha hizo ambazo sehemu zitakuwa mkopo na nyingine ufadhili, zitaelekezwa kwenye miradi mbalimbali iwapo mazungumzo ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Rais Macron na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta yatazaa matunda.
Rais Macron atatua nchini Machi13 na siku itakayofuatia, atahudhuria Makala ya nne ya Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (Unea-4) jijini Nairobi.
Hapo jana, Balozi wa Ufaransa nchini Aline Kuster alithibitisha kwamba ziara ya siku mbili ya Rais Macron italenga kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili.
“Usalama wa kitaifa, biashara, miundombinu na utunzaji wa mazingira ni baadhi tu ya mambo yatakayojadiliwa na wawili hao,” akasema Bi Kuster kwenye kikao na wanahabari katika makazi yake jijini Nairobi.
Wakati wa ziara hiyo, taasisi ya masomo ya juu huenda ikanufaika zaidi baada ya kubainika kwamba Marais hao watatia saini makubaliano matano ya kufadhili wanafunzi Wakenya kusomea Ufaransa na pia kupokezwa kazi nchini humo kulingana na kiwango chao cha masomo.
Mkuu wa Masuala ya Ushirikiano na Tamaduni Cyril Gerardon, alisema Kenya itapata mkopo wa Sh50bilioni na kuimarisha vyuo vyake vya kiufundi (TVET) mwaka wa 2019/20 na pia kuwezesha ubadilishanaji wa ujuzi wa kiufundi kati ya mataifa hayo mawili.
Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Kenya(TUK) na Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa(TUM) vitapokea ufadhili wa bure wa Sh48milioni kuimarisha mafunzo ya kozi za uhandisi, mpango ambao utadumu kwa miaka miwili na unaanza mwaka huu.
“Ufadhili huo utatekelezwa na Chuo Kikuu cha Paris Sud kama njia ya kushirikiana na kielimu na vyuo hivyo viwili vya Kenya,” akasema Bw Gerardon.
Zaidi ya Sh89milioni zitatumika kufadhili mtaala wa pamoja katika kitengo cha Sanaa ya ubunifu kitakachohusisha Taasisi ya kupokea habari kwa njia za kidigitali ya Afrika inayopatikana Nairobi na Chuo cha habari cha Rubika kutoka Ufaransa. Pesa nyingine zinazofikia kiwango cha Sh98milioni zitatumika katika shughuli za kuhifadhi mazingira nchini.
Rais Macron anazuru Kenya wakati kampuni za Ufaransa zimehusishwa na mpango wa kutwaa usimamizi wa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyataa(JKIA) kupitia Shirika la Ndege la Kenya Airways.