• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 1:05 PM
Wakenya wanaoishi Venezuela wataka kifo cha padri raia mwenzao kichunguzwe

Wakenya wanaoishi Venezuela wataka kifo cha padri raia mwenzao kichunguzwe

Na HILARY KIMUYU

Wakazi wa mji mmoja Mashariki mwa Venezuela sasa wanataka uchunguzi wa ndani ufanyike kuhusu kifo cha Padri Josiah Asa K’Okal ambaye ana mizizi yake Kenya.

Mwili wa Bw K’Okal ambaye alikuwa kati ya wanamishenari wa Consolata Venezuela, ulipatikana na maafisa wa usalama ukining’inia kwenye mti.

Mwili huo ulipatikana mtini kwenye msitu wa Guara, jimbo la Monagas mnamo Januari 2, siku moja baada ya kutoweka kwake.

Ripoti zinaarifu kuwa mwanamishenari huyo aliondoka kwenye makazi ya eneo la Paloma kunakoishi jamii ya Tucupita akiendesha baiskeli yake saa tatu asubuhi siku ya kwanza ya mwaka huu.

Akiondoka, aliacha simu yake na stakabadhi zake za kutambulishwa nyumbani kwake.

Alionekana mara ya mwisho saa tano mchana baada ya kutangamana na wenyeji kuanzia saa nne.

Kanisa hilo tayari limetoa taarifa za kusikitikia mauti ya padri huyo na kumwomba Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi.

“Ni kwa masikitiko makubwa tunatangaza kifo cha Papa Josiah Asa K’Okal ambaye alikuwa ametokomea tangu Januari 1, 2024,” ikasoma taarifa iliyotolewa na Wanamisheni wa Consolota Venezuela mnamo Januari 1, 2024.

“Tunaombea familia yake ipate nguvu ya kustahimili msiba huu na pia roho yake ilazwe mahala pema peponi,” ikaongeza taarifa hiyo.

Kanisa lilimrejelea Padri K’Okal kama mwanariadha, uzoefu ambao alipata alipokuwa Kenya. Mara nyingi alikuwa akishiriki mazoezi ya kukimbia, akiendesha baiskeli kwa masafa marefu ili kuzifikia parokia ambazo alikuwa ametwikwa jukumu la kusimamia.

“Ndugu tunaomba roho yako ilale mahala pema tena kwa amani. Ahsante sana kwa kuipenda Venezuela na kuwa mwanamisheni imara. Tunaomba Maria Consolata awe nawe kati ya wateule wake,” ikasema taarifa kwenye mtandao wa Wanamisheni.

Padri K’Okal alizaliwa mnamo Septemba 7, 1969 Kaunti ya Siaya, Nyanza. Alijitosa miongoni mwa wanamisheni wa Consolata mnamo 1993.

  • Tags

You can share this post!

FA: Mashabiki wa Manchester United kuganda na Arsenal

El-Nino imeua 174 kufikia Januari, ripoti ya majanga yasema

T L