Wakenya watakiwa kutoa maoni kuhusu "formula" iliyopitishwa na maseneta
Na CHARLES WASONGA
BUNGE la Kitaifa limealika wananchi kutoa maoni yao kuhusu mfumo wa mpya wa ugavi wa fedha baina ya serikali za kaunti uliopitishwa na Seneti Alhamisi, Septemba 17, 2020.
Kwenye tangazo lililochapishwa kwenye magazeti ya “The Saturday Nation” na “The Saturday Standard” bunge hilo linasema linataka maoni hayo ili kuiwezesha Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Bajeti kuidhinisha Mswada wa Ugavi wa Fedha baina ya Kaunti, (CARA).
Kuidhinishwa kwa mswada huo ambao pia ulipitishwa na Seneti Alhamisi, ndiko kutaiwezesha Hazina ya Kitaifa kuanzia kusambaza fedha kwa serikali zote 47 za kaunti.
“Ili kutimiza mahitaji ya vipengee vya 118 na 217 (4) vya Katiba, Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Bajeti sasa inaalika wananchi na wadau wengine kuwasilisha mapendekezo au maoni yoyote waliyonayo kuhusu Mfumo, wa awamu ya tatu, wa Ugavi wa Fedha baina ya Kaunti ulivyopitishwa na Seneti,” Bunge la Kitaifa lilisema katika notisi iliyotolewa na karani wa bunge hilo Michael Sialai.
Wananchi na wadau wengine wanahitajika kuwasilisha maoni yao kwa njia ya taarifa kwa afisi ya Karani wa Bunge la Kitaifa kupitia anwani zifuatazo: S.LP 41842-001100, Nairobi au barua pepe: [email protected]. Taarifa hizo pia zinaweza kuwasilishwa kwa Afisi ya Karani wa Bunge la Kitaifa, Orofa ya kwanza, Jengo Kuu la Bunge, Nairobi.
Mfumo huo mpya utatumiwa kugawa Sh370 bilioni ambazo Serikali za kaunti zinatarajia kupokea katika mwaka wa kifedha ujao wa 2021/2022, utakaoanza Julai 1, 2021.
Hata hivyo, katika mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021, maseneta walikubaliana kwamba mfumo wa mwaka jana utumiwa katika ugavi wa Sh316.5 bilioni zilizotengewa kaunti hizo. Kila kaunti itapokea kiasi cha fedha ilizopokea katika mwaka wa kifedha uliopita wa 2019/2020.
Chini ya mfumo mpya utakaanza kutekelezwa Julai 1, 2021, hakuna kaunti itapokea kidogo kuliko ilizopokea katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020, maseneta walisema katika hoja kuhusu mfumo huo.
Hoja hiyo iliwasilisha na Seneti wa Nairobi Johnson Sakaja, kwa niaba ya Kamati maalum ya maseneta 12 iliyotwikwa jukumu la kusaka muafaka kuhusu suala hilo.
Mfumo mpya unazingatia vigezo vinane vitavyotumika kugawanya fedha baina ya kaunti. Vigezo hivyo ni; ugavi sawa itachukua asilimia 20 ya fedha hizo, idadi ya watu (asilimia 18), afya (asilimia 17), viwango vya umasikini (aslimia 14), kilimo (asilimia 10), barabara (asilimia 8), ukubwa wa kieneo (asilimia 8) na uwepo wa miji (asilimia 5).
Inatarajiwa kuwa Bunge la Kitaifa litapitisha mfumo huo Jumanne, Septemba 22 sawa na mswada wa CARA.
Baadaye fomyula hiyo na mswada wa CARA zitarejeshwa katika seneta zipitishwa katika hatua ya mwisho kisha ziwasilishwe kwa Rais Uhuru Kenyatta azitie saini. Hapo ndipo, Msimamizi wa Bajeti (CoB) Margaret Nyakang’o atatoa idhini kwa Hazina ya Kitaifa ianze kusambaza fedha kwa kaunti.