• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Wakenya watatu wapinga kuvunjwa kwa Bunge

Wakenya watatu wapinga kuvunjwa kwa Bunge

Na RICHARD MUNGUTI

WAKENYA watatu Alhamisi waliwasilisha kesi katika mahakama kuu kupinga kuvunjwa kwa Bunge na Rais Uhuru Kenyatta kufuatia ushauri aliopewa na Jaji Mkuu David Maraga wiki hii.

Walalamishi hao watatu wanaomba suala hili lishughulikiwe kwa haraka kwa vile “ni sawa na kumega na kumeza ugali moto. Itachoma maini.”

Wakati huo huo, Jaji Weldon Korir alisikiza ombi la watatu hao na kuratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuifululiza moja kwa moja kwa Jaji Mkuu kuteua majaji wasiopungua watatu kusikiza malamishi yao. Kesi hiyo itatajwa Oktoba 7.

Jaji Maraga alikuwa amemshauri Rais Kenyatta avunje Bunge kwa vile ilishindwa kutunga na kupitisha sheria ya jinsia.

Sheria hii ingelipitishwa ingelishurutisha serikali inapoajiri watumishi wakuu wa umma izingatie mwongozo wa kuwatengea wanawake na walemavu thuluthi moja ya kazi za umma.

Wakili Andrian Kamotho Njenga pamoja na Mabw Leina Konchellah na Mohsen Abdul Munasah waliwasilisha kesi mbili tofauati wakiomba mahakama kuu iziratibishe kuwa za dharura na kusikizwa upesi na maamuzi kutolewa kuepusha nchi hii ikizama katika hali ya suinto fahamu na mtafaruku wa kikatiba.

Kesi hizo ziliwasilishwa katika mahakama kuu ya Milimani Nairobi.

Walalamishi hao Mabw Njena , Konchellah na Munasah wanasema “ ni za dharura”

Wakiomba mahakama kuu iingilie kati ya kuepusha nchi hii na suinto fahamu na mtafaruku wa kikatiba walalamishi hao wamekosoa ushauri huo aliotoa Jaji Maraga kwa Rais Kenyatta wakisema umepotoka na utaletea nchi hii madhara makubwa.

Wakili Njenga anasema katika kesi aliyowasilisha endapo Mahakama kuu haitaingilia kati na kutoa maagizo ya kumzuia Rais Kenyatta asitekeleze ushauri wa Jaji Mkuu atavunja Mabunge yote mawili bila kusita.

“Nchi hii itatumbukia katika mtafaruku wa kikatiba,” asema Bw Njenga katika ushahidi aliowasilisha kortini.

Huku akimshutumu Jaji Maraga kwa kutoa ushahuri uliopotoka na ulioko kinyume cha sheria kwa Rais Kenyatta, Bw Njenga amesema Bunge la Kitaifa na Bunge la Seneti hazikushtakiwa katika kesi sita ziliwasilishwa katika mahakama kuu katika kesi sita kuhusu utunzi wa sheria kuhusu jinsia.

“Jaji Mkuu amekiri katika ushauri aliotoa kwa Rais kwamba Mahakama kuu haikupeleka agizo kuhusu utunzi wa upitishaji wa sheria ya jinsia kama inavyotakiwa kikatiba na sheria,” asema

Wakili huyo amesema kwamba maagizo ya mahakama kuu yalipelekwa kwa Jaji Mkuu na walalamishi walioomba bunge ivunjwe kwa kushindwa kutekeleza jukumu lake.

Pia wakili huyo amesema ushauri aliotoa Jaji Maraga kwa Rais Kenyatta hautekelezeki kwa vile kinara huyu wa idara ya mahakama aliyumbishwa na kutoswa kando na sheria na walalamishi hawa.

“Bunge liko na majukumu makubwa na mamlaka makuu kisheria na kutokuwako kwa asasi hii ya pili ya Serikali itasabisha shughuli muhimu nchini kukwama,” alisema Bw Njenga.

Wakili huyo amemlaumu Jaji Maraga kwa kuchukua hatua hiyo kali kabla ya kuwapa wabunge wenyewe kueleza maoni yao kabla hajamshauri Rais Kenyatta kuwatimua wabunge kazini.

“Ushauri huu kwa Rais haujaeleza hatua itakayofuata baada ya Bunge kufungwa.Suala hili limesababisha mihemko mikali miongoni mwa wananchi,” asema Njenga.

Pia alisema hatua hiyo haikuzingatia matarijio ya kipengee namabri 35 (3) cha Katiba kinachosema kwamba Serikali itatangazia umma suala lolote litakaloathiri maisha yao kwa njia moja au nyingine.

Iwapo Rais ataivunja bunge kulingana na ushauri huo itakuwa vigumu kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuendeleza zoezi la uchaguzi.

Hii ni kwa sababu IEBC inakumbwa na uhaba wa Makamishna baada ya wanne wao kujiuzulu na haina afisa mkuu kufuatia kitimuliwa kazini kwa Ezra Chiloba.

Pia hakuna bajeti iliyotengewa uchaguzi mkuu mpya ikitiliwa maanani zoezi hili 2017 iligharimu Sh54bilioni.

Katika hoja zao Mabw Konchellah na Munasah wanadai hatua hiyo ya Jaji Maraga ni kuu kuliko mamlaka aliyo nayo.

Kupitia wakili Muturi Mwangi,wawili hawa wanadai ushauri huo wa kinara wa mahakama umepotoka kwa vile amechukua muda wa miaka mitatu kutojadilia suala hili la sheria za jinsia.

Wamesema kutekelezwa kwa ushauri huo kutaathiri utenda kazi wa serikali, na wapasa kusitishwa na mahakama kuu..

“Kesi hii inazua masuala mazito ya kisheria kuhusu mwelekeo kulingana na Kifungu nambari 261 na 261(7) cha Katiba,” asema Bw Mwangi.

Kwa mujibu wa vifungu hivi 261 Bunge limepewa jukumu la kutunga sheria kwa mujibu wa katiba na endapo haitafanya hivyo basi Jaji Mkuu atamshauri Rais aivunje.

Walalamishi hawa wanasema ushauri huu wa Jaji Mkuu utapelekea wakenya kuumia iwapo bunge litatimuliwa.

Katika kesi hiyo walalamishi wamemshtaki CJ na kuwataja Maspika wa Bunge la Kitaifa na Seneta na Mwanasheria Mkuu kama wahusika wakuu.

  • Tags

You can share this post!

Sharp Boys wapangia wapinzani vichapo

Red Carpet FC: Ukata unavyodidimiza azimio lake