Wakenya wazidi kuhatarisha maisha yao
Na WAANDISHI WETU
WAKENYA katika sehemu mbalimbali za nchi wanaendelea kukaidi maagizo yaliyotolewa na serikali kupambana na ueneaji wa virusi vya corona na kujiweka katika hatari ya kuambukizwa.
Uchunguzi wa Taifa Leo umeonyesha kuwa, licha ya idadi ya wagonjwa wanaoambukizwa virusi hivyo kuongezeka kila siku nchini, kuna Wakenya wengi ambao hawajali.
Masharti yanayokiukwa ni kama vile kutotoka nje wakati wa kafyu, kutokongamana na kuvalia barakoa wanapokuwa hadharani.
Kamishna wa Kaunti ya Mombasa, Bw Gilbert Kitiyo, alitaja wakazi wa maeneo ya Nyali, Kisauni, Changamwe na Likoni kama wanaongoza katika kuvunja sheria za kupambana na corona.
“Kuna vijana bado wanakongamana katika vikao vya miraa, wahudumu wa bodaboda pia wanakongamana katika vituo vya maegesho, kuna wazee wanaokusanyika katika vikao vya kahawa bila kujali wanahatarisha maisha yao na wengine,” akasema.
Katika maeneo ya Magharibi, wahudumu wa uchukuzi wa umma kuanzia boda boda hadi magari wameonekana kupuuza maagizo yaliyotolewa na serikali.
Uchunguzi katika Kaunti za Kakamega, Busia na Bungoma ulionyesha wengi wao hawapeani dawa za kusafisha mikono kwa wateja, matatu hazisafishwi na wenye matatu wanabeba abiria zaidi ya wanane.
“Siwezi tena kupata Sh300 kumpelekea mwajiri wangu kisha nibaki na hela za kutosha kutunza familia yangu. Hiyo yamaanisha sina pesa za kununua mahitaji yaliyotangazwa na serikali,” akasema Bw Salim Otuko, mhudumu wa boda boda katika eneo la Nambale, Kaunti ya Busia.
Katika Kaunti ya Kiambu, watu wapatao 76, wengi wao wakiwa vijana, walipatikana na polisi wakinywa pombe ndani ya baa usiku wakiwa wamejifungia.
Kamishna wa kaunti ya Kiambu, Bw Wilson Wanyanga, alisema wamiliki wa baa ambao wataendelea kukiuka sheria watapokonywa leseni zao, watengwe siku 14 kisha washtakiwe.
Na idara ya polisi Kaunti ya Trans-Nzoia ililalamikia ongezeko la wenyeji wa Kaunti hiyo wanaokiuka masharti ya kiusalama ya kusalia majumbani mwao saa za kafyu.
Kamanda wa polisi Kaunti hiyo, Bw Ayub Gitonga alisema wenyeji wengi hasa wale wa maeneo ya mabanda hukongamana nje baada ya saa moja jioni bila hata kuvaa maski.
Waendeshaji boda boda pia wanakaidi maagizo katika mitaa ya Kipsongo Tuwan Shimo la Tewa, Mitume, Lukhuna na Matisi ambapo pia wanaouza pombe hawajali sheria.
“Utasikia wakisema hapa Trans-Nzoia hakuna corona. Wewe unajuaje?” akasema.
Wakazi wa Kaunti ya Pokot Magharibi walilalamikia matumizi ya barakoa katika eneo hilo.
Walisema kuwa hawana fedha za kununua barakoa na wengi wao hawakusoma huku wengi katika maeneo ya mbali mashinani wakikosa kuelewa yanayoendelea.
Wakiongozwa na Bw Benjamin Lopuoyang, walitaka serikali isambaze barakoa hizo mashinani na pia viongozi wajitolee kuwaelimisha umma.
Na Osborn Manyengo, Lawrence Ongaro, Mishi Gongo, Shaban Makokha, na Oscar Kakai