Habari Mseto

Wakenya wengi hawafahamu yaliyomo kwenye ripoti ya BBI – Utafiti

December 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wengi hawafahamu yaliyomo kwenye ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) na wanaofahamu wanataka yatekelezwe kupitia kura ya maamuzi badala ya bunge, utafiti wa hivi punde wa shirika la Trends and Insight Africa (TIFA) unaonyesha.

Kulingana na utafiti huo, asilimia 69 ya Wakenya, wengi wao wakiwa wanawake walio na umri wa chini ya miaka 24, hawafahamu inavyosema ripoti hiyo.

“Kuna wanawake wengi wasiofahamu yaliyomo kwenye ripoti ya BBI kuliko wanaume. Wale walio na umri wa kati ya miaka 18 na 24 ndio wengi ikilinganishwa na wale walio na umri wa miaka 25 na zaidi,” TIFA inasema kwenye utafiti wake.

Utafiti unaonyesha kuwa Wakenya wanaoishi Nairobi na kaunti za eneo la Nyanza ndio wanaofahamu inavyosema ripoti hiyo kuliko wa maeneo mengine.

Nyanza ni ngome ya kiongozi wa ODM Raila Odinga aliyeasisi BBI pamoja na Rais Uhuru Kenyatta. Viongozi hao wawili walizindua ripoti hiyo jijini Nairobi Novemba 27, 2019.

Serikali iliahidi kuchapisha nakala za ripoti hiyo na kuzipeleka mashinani ili Wakenya wajisomee lakini wengi wanalalamika hawajazipata.

Kumekuwa na mdahalo kuhusu inavyopaswa kutekelezwa baadhi ya viongozi wakitaka iachiwe bunge huku wengine wakitaka kura ya maamuzi.

Ingawa wengi hawajaisoma ripoti hiyo, walisema wanataka iwasilishwe kwa Wakenya waipigie kura kwenye kura ya maamuzi.

“Ni chini ya asilimia 15 ambao wanahisi inapaswa kuachiwa wabunge waamue itakavyotekelezwa,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa TIFA, Maggie Ireri.

Asilimia 70 ya wakazi wa Nairobi na Pwani waliunga kura ya maamuzi, Nyanza ( asilimia 66), Rift Valley (asilimia 65), Kati (asilimia 56), Magharibi (asilimia 54) na Mashariki ( asilimia 53). Eneo la Kaskazini Mashariki asilimia 23 wanaunga kura ya maamuzi lakini asilimia 74 wanasema hawajui ripoti hiyo inavyopaswa kushughulikiwa.