Wakili afichua sababu ya kufungua wosia wa Cohen
Na RICHARD MUNGUTI
WAKILI mwenye tajriba ya juu aliyeandika na kuhifadhi wosia wa bilionea mwendazake Tob Cohen, Bw Chege Kirundi amesema hakuna kitu cha kuficha katika ugavi wa mali ya marehemu.
Bw Kirundi alisema jana kuwa ilibidi afichue alichoandika katika wosia huo kwa vile Cohen kwa dada yake na nduguye kwa vile alikuwa ameelezea jinsi angelitaka azikwe.
Wakili huyo aliyeanza kazi ya uwakili zaidi ya miaka 40 iliyopita aliwafungulia Bernard Cohen na Gabrielle Cohen Wosia huo katika sembule yake katika jengo la Bruce House Nairobi Ijumaa.
“Niliufungua wosia huo mbele ya ndugu yake marehemu, Bernard Cohen na dada yake Gabriele kuwasomea kwa vile mwendazake alikuwa ameelezea jinsi angelitaka azikwe katika makaburi ya Wayahudi kwenye barabara ya Wangari Mathai,” Bw Kirundi aliambia Taifa Jumapili/Sunday Nation kwa njia ya simu.
Alisema hakumfichulia mtu mwingine yeyote kuhusu wosia huo isipokuwa dada na ndugu ya marehemu.
“ Niliwapa Bernard Cohen na Gabrielle Cohen nakala ya wosia huo kile watakachofanya nao ndio wanajua,” alisema Bw Kirundi.
Wakili huyo alisema baada ya mazishi ya Tob Cohen kesho huenda mambo mengine aliyoandika katika wosia wake yakafichuliwa.
“Niliufungua wosia huo kwa mujibu wa sheria mbele ya dada yake na ndugu yake marehemu wajue alichosema kuhusu mazishi yake na ugavi wa mali yake,” alisema Bw Kirundi.
Wakili huyo alisema tayari Sarah Wairimu Kamotho kupitia kwa wakili wake Philip Murgor amesema ataupinga katika mahakama kuu.
Bw Murgor aliomba mahakama imwachilie Sarah anayeshtakiwa kwa mauaji ya Cohen kwa dhamana akapiganie mali yake.
“Namtakia kila laheri Sarah katika jitihada zake za kupinga wosia wa mumewe kuhusu ugavi wa mali yake,” alisema Bw Kirundi.
Sarah alisema hayo baada ya vyombo vya habari kuripoti Cohen alikuwa amempa dada yake Gabrielle jumba lake la kifahari iliyoko mtaa wa Kitsuru lenye thamani ya Sh400 milioni.
Bw Murgor alilalamika mbele ya Jaji Jessie Lesiit kwamba asili mia 50 ya mali ya marehemu ni ya Sarah.
Bw Murgor alimweleza Jaji Lesiit kwamba kuna kesi ya talaka inayoendelea mahakamani na “ suala nyeti ni mali.”
Cohen alitoweka Julai 19/20, 2019 na maiti yake ilipatikana wiki iliyopita ikiwa imetupwa ndani ya tangi la maji taka katika makazi yake.
Sarah hajajibu shtaka lakini anaomba afisa mkuu wa gereza la wanawake la Langata Nairobi aagizwe ampeleke katika makaburi ya wayahudi ahudhurie mazishi ya mumewe na kutoa heshima zake za mwisho.
Sarah atajibu shtaka la kumuua mumewe Septemba 26 na siku hiyo ataomba aachiliwe kwa dhamana.
Viongozi wa mashtaka Nicholas Mutuku, Aelxander Muteti na Catherine Mwaniki walimweleza Jaji Lesiit watapinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.
Mahakama itaamua kesho ikiwa Sarah atasindikizwa kuhudhuria mazishi ya mumewe. Mazishi ya Cohen ni ya kibinafsi.Itahudhuriwa na watu wa familia yake peke yao.
Mawakili Cliff Ombeta na Dunstan Omari walikuwa miongongi mwa watu waliohudhuria zoezi la kusomwa kwa wosia huo.
Bw Murgor anayemwakilisha Sarah pamoja na George Ouma hakuwakuhudhuria zoezi la kufunguliwa na kusomwa kwa wosia wa Cohen.