• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
Wakili kizimbani kwa kuiba mamilioni ya mteja wake

Wakili kizimbani kwa kuiba mamilioni ya mteja wake

Na RICHARD MUNGUTI

WAKILI aliyepokea pesa za pensheni ya mfanyakazi wa shirika la ustawishaji maji na mabomba (NWPC) aliyetimuliwa kazini ameshtakiwa kwa wizi wa Sh5.8m.

Bw Evans Asuga Ongichi alishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Bi Zainab Abdul Ijumaa.

Bw Ongichi alikana alimwibia mteja wake Bw Misheck Mokua Saboke Sh5,858,080 alizopokea kwa niaba yake kutoka kwa NWPC.

NWPC ilikuwa imeamriwa na mahakama ya rufaa imlipe Bw Saboke pesa hizo Sh5.8m kwa kutimuliwa kazini kimakosa.

Mahakama ilifahamishwa wakili huyo alipokea pesa hizo kati ya Oktoba 17 2019 na February 5 2020.

Wakili huyo aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana akisema “nimekuwa nje kwa dhamana ya polisi ya Sh200,000.”

Bw Ongichi aliomba mahakama izingatie yeye ni afisa wa korti na “anajua athari za kutofika kortini siku ya aidha ya kutajwa kwa kesi inayomkabili ama siku ya kusikizwa.”

Mahakama ilimwachilia wakili huyo kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh200,000.

Mshtakiwa huyo aliiba pesa hizo zilipowekwa katika akaunti ya afisi yake ya Ongicho Ongicho iliyo katika Benki ya Equity.

Bi Abdul aliamuru kesi hiyo itajwe baada ya wiki mbili kuwezesha upande wa mashtaka kumkabidhi wakili huyo nakala za mashahidi.

“Kuna jitihada za kusuluhisha kesi hii nje ya mahakama. Ikiwa mashauri haya yataleta maafikiano basi tutaomba mahakama itamatishe kesi ikiwa mshtakiwa atakuwa amemlipa mlalamishi pesa zake zote,” hakimu alifahamishwa.

Kesi itatajwa Novemba 24, 2020.

  • Tags

You can share this post!

Rais Kenyatta amwokoa Leonard Mambo Mbotela

Duncan Otieno ayoyomea Zambia