Habari Mseto

Wakili taabani kwa kughushi mali ya mtalikiwa

August 8th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

WAKILI alishtakiwa Jumanne kwa kumsaidia mume aliyemtaliki mke kulaghai ardhi yenye thamani ya Sh10 milioni katika kaunti ya Kajiado.

Bw Alex Kibunja Ngure alikanusha shtaka la ughushi wa ardhi iliyoko eneo la Kitengela iliyomilikiwa na Bw Dominic Kibathi na kuiandikisha kwa jina la Bi Jane Kibathi Njoroge.

Bw Ngure alikanusha kughushi hatimiliki ya shamba hilo lenye thamani ya Sh10milioni.

Wakili Winstone Ngaira aliomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana akisema kuwa , “mshtakiwa ni wakili aliyekuwa akiwatetea Bw na Bi Kibathi katika kesi ya talaka miaka mitano iliyopita.”

Bw Ngaira alimweleza hakimu kuwa mshtakiwa alikuwa anawatetea washtakiwa hao “ na hakuhusika kamwe na ugavi wa mali yao.”

Bw Ngaira aliambia mahakama kuwa Bi Jane Kibathi Njoroge ni mkewe, Dominic na amehamia Uingereza.

“Nitawasilisha ushahidi kutoka mahakama kuu kuthibitisha jinsi mshtakiwa alikuwa anawatetea mume na mke huyu  waliotengana,” alisema Bw Ngaira.

Mahakama ilielezwa kuwa mshtakiwa sio msajili wa ardhi eti alibadilisha umiliki wake.

Hakimu alielezwa kuwa mshtakiwa alitiwa nguvuni kutoka mahakama ya Kiambu kama “ mhalifu na kuzuiliwa katika kituo cha polisi kabla ya kufikishwa kortini.”

Hakimu alikabidhiwa nakala ya cheti cha uwakili cha mshtakiwa alicholipa mwaka huu.

“Naomba mahakama imwachilie mshtakiwa kwa dhamana. Ni wakili na hatakuwa na budi ila kufika kortini,” Bw Ngaira alimweleza hakimu mkazi Bi C M Nzibe.

Ombi la kuachiliwa kwa dhamana lilipinga na wakili wa Serikali Bi Georgina Mwangi aliyesema “ hakuna ushahidi wowote uliotolewa mahakamani kuthibitisha mshtakiwa alikuwa akiwakilisha mume na mke huyo katika kesi ya talaka.”

Hakimu aliamuru mshtakiwa azuiliwe kabla ya uamuzi wa dhamana kutolewa.