Habari MsetoSiasa

Wakulima wa miwa wamtaka Kiunjuri ajiuzulu

November 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RUTH MBULA

WAKULIMA wa miwa wanamtaka Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri ajiuzulu wakidai ameshindwa kusuluhisha changamoto zinazokumba sekta hiyo.

Wakulima hao, wamelalamika kwamba wanazidi kuteseka kwa malipo duni yanayosababishwa na sukari ya bei ya chini inayoingizwa nchini kutoka mataifa ya nje.

Kwenye taarifa, walisema wafanyabiashara matapeli wamezidi kudhibiti sekta hiyo huku mkulima anayefanya kazi ngumu shambani kuzalisha miwa akiendelea kutaabika.

Maafisa wa Shirikisho la Wakulima wa Miwa Kenya wakiongozwa na Mwekahazina wa Kitaifa, Bw Stephen Narupa, walisema kutokana na kuwa viwanda vya serikali magharibi mwa Kenya vimefilisika, wakulima wamelazimika kugeukia viwanda vya kibinafsi ambavyo haviwafaidi.

“Tumeuliza wamiliki wa viwanda vya kibinafsi kwa nini hatulipwi vizuri , wakasema ni kwa vile kuna sukari chungu nzima ya bei nafuu kutoka nchi za kigeni sokoni,” akasema Bw Narupa.

Bei ya miwa kwa wastani sasa ni Sh3,500 kwa kila tani, kutoka Sh4,300 ilivyokuwa miezi miwili iliyopita.

Uagizaji sukari kutoka nchi za kigeni ulipanda kwa asilimia 102 kufikia Juni mwaka huu.

Wasimamizi wa viwanda vya kibinafsi vya kutengeneza sukari pia wamekuwa wakipinga uagizaji sukari za bei ya chini kutoka nchi za kigeni wakisema hali hiyo inadhuru wadau wa sekta hiyo humu nchini.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Sukari ya Trans Mara, Bw Fredrick North Coombs, alisema licha ya kuwa serikali ilikamata Wakenya wengi mwaka uliopita wakihusishwa na uagizaji sukari kinyume cha sheria, bado kuna kiwango kikubwa mno cha sukari hiyo sokoni.

Bw North alisema hali hiyo ndiyo inaumiza wakulima kote nchini huku akionya kwamba changamoto zinazokumba sekta ya sukari zitazidi kushuhudiwa kama serikali haitadhibiti kikamilifu uagizaji bidhaa hiyo kutoka mataifa ya kigeni.

Magavana wa kaunti zinazotegemea kilimo cha miwa kimapato, pia wamekuwa wakipinga mpango wa kuagiza sukari kutoka Uganda, hatua inayodaiwa inataka kuchukuliwa ili kuzuia uhaba wa sukari nchini.

Ripoti kutoka kwa Idara ya Sukari inaonyesha kati ya Januari na Juni mwaka huu, tani 200,442 za sukari ziliingizwa nchini. Kiwango hicho ni kikubwa kikilinganishwa na tani 99,144 za mwaka jana.