• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:07 PM
Wakuu wa fedha na ununuzi serikalini watupwa nje

Wakuu wa fedha na ununuzi serikalini watupwa nje

Na VALENTINE OBARA

MAMIA ya watumishi wa umma wamesimamishwa kazi kwa muda kufuatia agizo lililotolewa na Rais Uhuru Kenyatta wakati wa sherehe za Madaraka Dei mwishoni mwa wiki iliyopita.

Msemaji wa serikali jana alithibitisha kuwa maafisa wote wakuu wanaosimamia idara za uhasibu na ununuzi katika wizara zote na mashirika ya serikali wamepewa likizo ya lazima ya siku 30 ili wafanyiwe uhakiki upya.

Kama njia mojawapo ya kupambana na ufisadi serikalini, Rais Kenyatta alikuwa ameagiza uhakiki huo ufanywe kwa kutumia mashine zitakazotambua kama watumishi wa umma watakuwa wanasema ukweli watakapohojiwa upya.

Taarifa iliyotumwa na Msemaji wa Wizara ya Ndani Mwenda Njoka kwa niaba ya Msemaji wa Serikali Eric Kiraithe, ilisema maafisa hao watatakikana kupeana mamlaka yao kwa manaibu wao kisha waondoke afisini mara moja.

“Rais amejitolea kuunda utumishi wa umma unaotumikia mahitaji ya Wakenya bila watu kutumia mamlaka yao kujitajirisha kibinafsi,” ikasema taarifa hiyo.

Watahitjika kuwasilisha habari zao za kibinafsi kwa Afisi ya Mkuu wa Utumishi wa Umma ifikapo Ijumaa.

Ilibainika masuala yatakayolengwa katika uhakiki ni kuhusu kiwango cha mali wanazomiliki na mienendo yao ya awali ya kikazi.

“Ingawa shughuli hii inalenga kutambua kama watumishi wa umma wanastahili kuendelea kuhudumu, na kuimarisha imani ya wananchi kwa utumishi wa umma, itafanywa kwa njia ya haki kwa kuzingatia haki za maafisa hao kama ilivyo kwenye katiba,” Bw Njoka alieleza.

Kuna zaidi ya mashirika 110 ya serikali nchini zinazohudumu chini ya wizara 22 zilizopo na inatarajiwa kila shirika lina kitengo cha uhasibu na cha ununuzi zinazosimamiwa na watu tofauti.

Rais Kenyatta amekuwa akisisitiza kuwa serikali yake haitavumilia kuwa na wafanyakazi ambao hufuja mali ya umma kupitia kwa ufisadi.

Ari yake ya kupambana na ufisadi katika kipindi chake cha pili na cha mwisho cha uongozi imezidi kushuhudiwa kufuatia msururu wa sakata za ufisadi ikiwemo katika shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) ambapo washukiwa zaidi ya 20 walifikishwa mahakamani kufikia Jumatatu.

Juhudi hizo zimepigwa jeki na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga, ambaye aliunga mkono msimamo wa rais kwamba washukiwa wa ufisadi wakome kujificha chini ya vyama vya kisiasa na makabila yao wanaponaswa.

Mashirika mengine ambapo kumeibuka sakata za ufisadi hivi majuzi ni Shirika la Usambazaji Umeme nchini (Kenya Power), Bodi ya Kitaifa ya Mazao na Nafaka (NCPB) na Shirika la Mafuta nchini (Kenya Pipeline).

You can share this post!

Walimu wachunguzwa kuhusiana na visa vya ubakaji shuleni

Niteue niwe naibu wako, Passaris amrai Sonko

adminleo