Wakuu wa Kemsa wasimamishwa kazi kufuatia sakata ya pesa za corona
Na BENSON MATHEKA
AFISA Mkuu Mtendaji wa shirika la serikali la kusambaza dawa – Kenya Medical Supplies Authority (KEMSA) – Jonah Manjari Mwangi na maafisa wengine wawili wamesimamisha kazi kufuatia madai ya ukiukaji wa kanuni za kununua bidhaa za kujikinga na virusi vya corona.
Uchunguzi unaendelea kubaini jinsi shirika hilo lilivyotoa zabuni za zaidi ya Sh100 bilioni zilizopatiwa Kenya na wafadhili kusaidia vita dhidi ya janga la corona nchini.
Kulingana na mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo, Kembi Gitura, Dkt Mwangi alisimamishwa pamoja na mkuu wa idara ya ununuzi wa bidhaa Charles Juma na Mkurugenzi wa shughuli za Kibiashara Eliud Mureithi ili Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) ikamilishe uchunguzi kuhusu suala hilo.
Bodi imemteua mkurugezi wa mipango Edward Njoroge Njuguna kuwa kaimu Afisa Mkuu Mtendaji.
Bw Edward Buluma atakuwa kaimu mkuu wa idara ya ununuzi na Dkt George Walukana ashikilia wadhifa wa mkurugezi wa biashara.
Hatua hii ilijiri baada ya kufichuliwa kwamba huenda maafisa wa KEMSA walikiuka kanuni za ununuzi kwa kutoa zabuni ya kima cha Sh4 bilioni moja kwa moja kwa kampuni inayofahamika kama Kilig Limited.
Kampuni nyingine zilipatiwa tenda za mamilioni pesa kabla ya kutimiza miezi sita baada ya kusajiliwa.
Tenda hizo zilitiliwa shaka baada ya kuibuka kuwa kampuni ziliuza vifaa kwa bei ya juu kuliko ya kawaida.
Kwa mfano, kampuni moja iliuzia shirika hilo barakoa aina ya KN95 kwa Sh700 ilhali bei ya kawaida ni Sh450.
Maafisa wa shirika hilo wamejitetea wakisema bei ilikuwa juu kufuatia uhaba wa vifaa hivyo ulimwenguni walipotoa zabuni hizo.