• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Wakuu wa KPC kizimbani kwa ufujaji wa mabilioni

Wakuu wa KPC kizimbani kwa ufujaji wa mabilioni

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI mkuu wa kampuni ya Kenya Pipeline Company (KPC) alishtakiwa Jumatatu kwa matumizi ya Sh1.9 bilioni kiholela.

Bw Joe Kimutai Sang alishtakiwa wakati polisi wanaendelea kuchunguza kashfa inayohusisha zaidi Sh13 bilioni katika KPC.

Kwa ujumla polisi wanaendelea kumulika jinsi zaidi ya Sh60 bilioni zilivyotumika.

Bw Sang aliyetiwa nguvuni mwishoni mwa wiki jana alifikishwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bw Douglas Ogoti.

Bw Sang alishtakiwa pamoja na  Bi Gloria Robai Khafafa , Bw Vincent Korir Cheruiyot, Bw Billy Letuny Aseka, Bw Nicholas Gatobu na Bw Samuel Odoyo.

Wote walikabiliwa na shtaka la kujenga kituo cha kusambaza bidhaa za mafuta ya petrol cha Kisumu Oil Jetty pasi na mpango.

Shtaka lilisema wakuu hao wa KPC walisababisha KPC kutumia Sh1,963,065,422 kinyume cha sheria.

Mahakama ilifahamishwa kuwa washukiwa hao waliidhinisha matumizi ya pesa kabla ya kukadiriwa katika bajeti ya matumizi ya KPC.

Mabw Sang (mkurugenzi mkuu) , Cheruiyot (meneja mkuu masuala ya fedha) , Aseka (meneja mkuu wa masuala ya ununuzi bidhaa), Gatobu (mhandisi) , Odoyo na Bi Khafafa walishtakiwa kuidhinisha ujenzi wa kituo cha  Kisumu Oil Jetty kilichogharimu  shirika hilo Sh1,963,065,422 bila idhini.

Bw Sang alikabiliwa na shtaka la kutumia mamlaka yake vibaya kwa kuidfhinisha ujenzi wa Kisumu Oil Jetty utekelezwe na kampuni ya Southern Engineering Company Limited (SECL) na kupelekea KPC kutumia bila mpango Sh1,963,065,422.

Mbali na shtaka hilo , Bw Sang alikabiliwa na mashtaka mengine matatu ya kufuja pesa za umma kupitia mradi huo wa Kisumu Oil Jetty.

Bi Khafafa ambaye alikuwa wakili mkuu wa KPC alishtakiwa kwa kutumia mamlaka ya afisi yake vibaya na kupelekea KPC kupoteza Sh1,963,065,422.

Bw Korir akiwa meneja mkuu masuala ya ununuzi wa bidhaa alishtakiwa kutumia mamlaka ya afisi yake vibaya kwa kuidhinisha malipo ya kwa ujenzi wa mradi huo Kisumu Oil Jetty kinyume cha sheria.

Kwa jumla washtakiwa walikana mashtaka sita na wakili Ahhamednassir Abdullahi kuomba washukiwa hao waachuliwe kwa dhamana.

Bw Abdullahi alisema kuwa mashtaka yaliyowasilishwa dhidi ya washtakiwa hayalingani na kiwango cha pesa kinachodaiwa kilitoweka katika kampuni .

“Washtakiwa hawa hawakuhusika kwa ufujaji wa pesa za KPC kupitia ujenzi huo ila waliisaidia katika kufanikisha utenda kazi wake,” alisema Bw Abdullahi.

Upande wa mashtaka uliongozwa na naibu wa mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma (ADPP) Bi Emily Kamau.

Kila mmoja wa washtakiwa hao aliachiliwa kwa dhamana ya Sh2milioni pesa tasilimu.

Kesi itatajwa baada ya wiki mbili kutengewa siku ya kuisikiza.

You can share this post!

Torreira atajwa injini ya kuimarika kwa Arsenal

UPORAJI: Mamilionea bila jasho

adminleo