Habari Mseto

Wakuzaji miwa walia kampuni kufungwa ghafla

November 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na VICTOR RABALLA

Wakulima wa miwa Alhamisi walisema kufungwa ghafla kwa kampuni ya sukari ya Kibos kumewaacha taabani.

Wakulima hao walikosoa hatua hiyo kwa kusema hawana soko la kupeleka miwa yao.

Walitaja hatua hiyo ya Jumatano na Mahakama Kuu ya Kisumu kali sana, ambayo itawafanya kupata hasara kubwa kutokana na kuwa waliachwa na tani nyingi za miwa ambazo tayari zimekatwa.

Shirikisho la vyama vya wakulima wa miwa nchini (KNFSF) lilishutumu mahakama hiyo kwa kukataa kuzingatia maslahi ya wakulima.

Mahakama hiyo ilitoa agizo la kufungwa kwa kampuni hiyo kwa siku 14 kwa kushindwa kutekeleza kanuni za kimazingira.

“Zaidi ya tani 50,000 za miwa zinazidi kuharibika baada ya kuvunwa na zingine zimo kwa tinga tinga katika madaraja ya kupima uzani,” alisema mwenyekiti wa shirikisho hilpo Jeckonia Oyoo.

Bw Oyoo alisema hatua hiyo itawafanya wakulima wa miwa maskini, kwa kuzingatia kuwa kampuni za sukari za Chemilil na Muhoroni hazifanyi kazi kwa kiwango kikubwa.

Alisema shirikisho hilo litaomba kujumuishwa katika kesi hiyo kwa lengo la kuwakilisha wakulima ambao wamepuuzwa katika kesi hiyo.

Katibu Mkuu wa Chama cha wakulima wa miwa Kaunti ya Kisumu Richard Ogendo alisema suala hilo linafaa kusuluhishwa kwa njia nzuri, ikizingatiwa kuwa sekta ya miwa imetoa ajira kwa idadi kubwa zaidi ya wakazi wa eneo hilo.

“Uamuzi wa mahakama ulifaa kuwa wa haki kwa lengo la kuipa Kibos wakati wa kutumia miwa iliyokuwa imevuna huku ikizidi kutekeleza matakwa,” alisema katibu mkuu wa KNFSF Bw Ezra Okoth.

Mwekahazina wa shirikisho hilo Bw Stephen ole Narupa aliomba serikali kuwasaidia wakulima wa miwa kuwaepushia hasara.