Walalama mazao yanaozea mashambani sababu ya barabara mbovu
Na SAMMY WAWERU
KIRINYAGA ni miongoni mwa kaunti ncini Kenya ambazo zimetia fora kwenye kilimo ikizingatiwa kwamba ina aina nzuri ya udongo na pia ina hali nzuri ya hewa.
Inafahamika katika ukuzaji wa mpunga-unaozalisha mchele, hasa eneo la Mwea.
Pia, Kirinyaga ni mkuzaji wa ndizi, kahawa, majani chai na nyanya.
Licha ya kuwa na sifa kuntu katika kilimo, baadhi ya maeneo wakazi wanalalamikia miundo msingi duni.
Wakulima eneo la Karii, wadi ya Kangai, eneo la Mwea, wanalalamikia mazao yao yamekuwa yakiozea mashambani kwa sababu ya barabara duni ambazo hazipitiki msimu wa mvua.
Eneo hilo ni tajika katika ukuzaji wa ndizi, nyanya, mboga na Maharage ya Kifaransa.
“Msimu kama huu wa mvua tunakadiria hasara isiyomithilika, barabara hazipitiki kwa kuwa ni mbovu,” mkazi akateta, wakati wa mahojiano na Taifa Leo.
Katika hafla iliyoandaliwa Karii wiki hii na H.M Clause, kampuni inayounda mbegu za mimea kama nyanya, mboga, matikitimaji, pilipili mboga, iliyolenga kutoa mafunzo bora ya kilimo, Erastus Muriuki Kamau alisema si mara moja mazao yake yameharibikia shambani kwa sababu ya barabara zisizopita wakati wa mvua.
Alilalamika kwamba amekadiria hasara ya mazao yenye thamani ya mamilioni ya pesa.
“Eneo hili lina viongozi tuliochagua kama vile diwani (MCA), tunachoomba serikali ni itutengenezee barabara la sivyo huenda kilimo kikawa kigumu kufanya,” alisema Bw Muriuki.
MCA wa Kangai ni Bw John Gitari, naye Anne Waiguru akiwa Gavana wa Kaunti ya Kirinyaga.
Wakazi wanasema malalamishi yao yamepuuzwa, huku wakiendelea kukadiria hasara.
Nyingi ya barabara eneo hilo ni za kutandazwa na msimu wa mvua magari hukwama kwa sababu ya udongo. Walilalamika pikipiki na ambazo zimerahisisha shughuli za usafiri na uchukuzi, hulemewa kuingia humo.