Walazwa baada ya kula matawi ya mmea unaokisiwa kuwa na sumu
Na SHABANA MAKOKHA na CHARLES WASONGA
WATU watano wa familia moja kutoka mtaa wa Mjini, Mumias wamelazwa hospitalini baada ya kula matawi ya mmea unaokisiwa kuwa na sumu.
Bi Samla Atieno na wanawe wanne walikula matawi ya mmea huo walioyachanganya na mboga za kienyeji kisha kupika mnamo Alhamisi.
“Tumekuwa tukila matawi na mmea huu kwa muda mrefu. Niliyachanganya matawi hayo na mboga aina na ‘managu’ lakini baada ya kula tulipoteza fahamu,” akasema Bi Atieno akiwa katika wadi kwa jina Teresa katika Hospitali ya St Marys Mumias.
Watoto wake watatu wenye umri wa miaka minne na minane wamelazwa katika wadi ya watoto, huku ndugu yao mkubwa, Abubakar Gunga, 18, akilazwa katika wadi ya wanaume.
“Nilikuwa kazini nilipopigiwa simu na jirani aliyeniambia kuwa familia yangu anaugua,” akasema Bw Hassa Gunga ambaye ni baba ya watoto hao.
Alisema mkewe alikuwa amechanganya mabaki ya chakula walikuwa Jumatano na chakula kingine kisha atawaandaliwa wanawe Alhamisi mchana.
“Nadhani hii ndio chanzo cha shida, kwani tumekuwa tukila mboga hizo kwa muda mrefu na hatujawahi kutatizika kwa njia yoyote. Hata hivyo, nasubiri ripoti ya madaktari ili kujua chanzo cha shida hiyo,” Bw Gunga akaongeza.
Hata hivyo, Dkt Protus Mate ambaye ni daktari wa watoto alisema familia hiyo iliathiriwa na sumu kutokana kwa mmea unaojulikana kisayansi kama Datura stramonium.
“Ni mmea wenye sumu ambao husababisha mtu kupoteza fahamu. Sumu yake husambaa kwa mwili haraka na ni bahati nzuri kwamba waathiriwa waliletwa hapa haraka,”akasema Dkt Mate.
Alisema wagonjwa hawako hatarini baada ya kupewa matibabu, iliyohusishwa kuondolewa kwa sumu mwilini mwao.
“Ni mtoto mmoja tu ambaye bado anaonyesha dalili za kuchanganyikiwa huku macho yakiwa hayaoni vizuri,” Dkt Mate akaongeza.