Habari Mseto

Walimu Thika watetea maslahi yao

July 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

CHAMA cha walimu nchini (Knut) tawi la Thika, kimeiomba serikali iangalie upya maslahi ya walimu ikizingatia kazi muhimu wanayotekeleza.

Bw James Ndiko ambaye ni naibu mwekahazina wa chama kikuu cha Knut nchini amewahimiza wasilegeze kamba bali wawe mstari wa mbele kutetea haki yao.

Naibu mwekahazina wa kitaifa wa Knut, Bw James Ndiko ahutubia walimu Julai 6, 2019, mjini Thika. Picha/ Lawrence Ongaro

“Kitu cha kwanza ni sharti ufurahie kuwa mwalimu kwa sababu hicho ndicho kipaji chako maishani,” akasema Bw Ndiko.

Aliwahimiza walimu wawe kitu kimoja na wasikubali kutenganishwa kuwa vikundi tofauti.

Alisema Wizara ya Elimu ni sharti ifanye kazi pamoja na chama cha Knut ili kufanya mabadiliko ifaayo katika chama hicho.

“Chama cha Knut kitakuwa imara na hakitakubali kutenganishwa. Chama hicho kimetetea walimu kwa muda mrefu na hakingekubali kuona ya kwamba kinatenganishwa,” alisema Bw Ndiko.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki mjini wa Thika wakati wa mkutano wa pamoja wa kila mwaka.

Alisema mpango wa serikali wa kuwahamisha walimu hadi katika sehemu za mbali ni hatari, na unastahili kujaadiliwa kwa makini.

“Sio vibaya kuhamishwa, lakini kuna mambo mengi ambayo yanastahili kuchunguzwa, kabla ya kufikia uamuzi huo,” alisema Bw Ndiko.

Barua rasmi

Alisema iwapo mwalimu yeyote yule atajisikia kuwa anataka kuhamishwa, bila shaka hafai kukatazwa mradi tu ameandika barua rasmi.

Alizidi kueleza ya kwamba kuna walimu ambao umri wao umesonga, wengine wana matatizo ya kiafya, huku wengine wakiwa na familia wanaoishi nao pamoja.

Kwa hivyo alidai maswala hayo yote yakitiliwa maanani bila shaka kutakuwa na uelewaano mzuri kati ya serikali na walimu.

Alitaja taaluma ya ualimu kuwa ni yenye umuhimu mkubwa kwa sababu mwalimu ni mtu anayeondoa ‘ujinga’ kwa mwanafunzi na kumjenga kuwa mtu wa kutegemewa.

Alipendekeza walimu wanaostaafu kupewa muda wa miezi sita mapema ili serikali nayo iwe ikitayarisha marupurupu yao.

“Kwa muda mrefu sasa walimu wengi ambao hustaafu hupitia masaibu mengi wanaporudi makwao wakisubiri haki yao ya fedha. Jambo hilo limewafanya walimu hao waliostaafu kuingilia kazi duni za kujikimu, nyingi zikiwa ni za sulubu,” alisema Bw Ndiko.