Walimu wa JSS: Tulivyoteseka, ni mgomo tu ungefanya tusikizwe
WALIMU wa Shule za Sekondari Msingi (JSS) katika Kaunti ya Kilifi, wameeleza masaibu ambayo wamekuwa wakiyapitia kazini.
Bi Stacy Munga, mwalimu katika mojawapo ya shule huko Vuga katika maeneo ya mbali ya Kaunti ya Kilifi, alisema si tu kwamba wanafanya kazi katika hali ngumu, bali pia mishahara yao huchelewa sana.
“Nilipelekwa katika shule hiyo peke yangu mnamo Februari nikiwa na wanafunzi 67. Nilifundisha masomo 14 na tulilazimika kukaa kwa miezi kadhaa kabla ya kupata mshahara wetu wa kwanza. Tuliishi kwa mikopo,” alisema.
Bi Munga alisema shule hiyo iko ng’ambo ya pili mto na kuna barabara mbovu ya kupitia kabla ya kufika kazini. Alisema anatumia karibu Sh200 kutoka Kaloleni hadi shuleni na wakati wa mvua lazima asubiri maji ya mto yapungue kabla ya kuvuka kwenda shuleni.
“Sikuwa na kazi kwa zaidi ya miaka mitano. Tulikubali kuvumilia maisha magumu kwa sababu ya watoto ambao kila mara wanatugusa mioyo na sasa tunaumia kwa sababu hatuwafundishi,” alisema.
Bi Munga alisema inakatisha tamaa kuwa mtu mwenye shahada ya kwanza anafanya kazi katika hali ngumu ilhali wale wenye stashahada ambao wanafanya nao kazi pamoja wana ajira ya kudumu iliyo na pensheni.
Bi Munga alitoa changamoto kwa serikali kujitokeza wazi kuhusu mpango wake wa kuwapa ajira vijana wengi waliohitimu nchini.
“Mwalimu katika Kaunti ya Kilifi anapokea kipato kidogo ikilinganishwa hata na mhudumu wa bodaboda mwenye umri wa miaka 16 na hata mgema wa mnazi,” alisema.
Bw Andrew Lelei, ambaye pia ni mwalimu wa JSS, alisema serikali haiwatendei haki na haikuwa mwaminifu kwao.
“Sisi ndio waanzilishi wa CBC na kwa hivyo, hatujifunzi kutoka kwa mtu yeyote. Serikali ituthibitishe kuwa walimu wa kudumu na wanaolipwa pensheni na pia kutufidia,” alisema.
Bw Lelei alisema kwamba alisaidiwa kuendeleza elimu ya chuo kikuu na kanisa lake la mtaani na kwamba yeye ndiye mlezi wa familia yake.
“Kanisa lilichangia elimu yangu ya chuo kikuu na hivyo kila kunapokuwa na harambee wanategemea nipeleke michango yangu na huwa nikipokea barua za mwaliko, lakini fedha hizo hazitoshi kwangu mimi, familia yangu na kusaidia wale walioniwezesha kusoma,” alisema.
Walimu hao walikuwa wamekwenda kuwasilisha malalamiko yao kwa Mkurugenzi wa Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) wa Kaunti ya Kilifi, Bw Edward Zani Mwazani.
Mkurugenzi huyo wa TSC aliwataka walimu hao kurejea kazini na kusubiri Serikali ya Kitaifa kushughulikia lalama zao. Bw Mwazani alisema serikali inafahamu hali ya sasa ya shuleni.
“Tatizo hili halitatatuliwa katika ngazi ya kaunti. Nawaomba muende kazini muwe na subira,” alisema.