Habari Mseto

Walimu wa madrasa wahimiza wazazi watumie teknolojia kusomesha watoto elimu ya dini

May 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MISHI GONGO

WALIMU wa madrasa wamewashauri wazazi kutumia mitandao kuwasomesha watoto wao msimu huu ambapo shule hizo za elimu ya Kiislamu zimefungwa kufuatia kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19.

Akizungumza na Taifa Leo Bw Fadhili Thabit mwalimu wa shule ya madrasa Magongo amesema kufuatia kufungwa kwazo, watoto wengi wamekuwa wakirandaranda mitaani huku wakitelekeza masomo ya dini.

Sasa amewashauri wazazi kutumia mitandao kuwaendeleza watoto wao ili kuhakikisha hawasahau waliyofunzwa.

“Hii ni likizo ndefu ambayo hatujui itamalizika lini, hivyo kuna uwezekano wa watoto kusahau waliyofunzwa hivyo ni vizuri mzazi akamhimiza mwanawe kusoma kupitia mitandao,” akasema.

 

 

Mosab Abdallah, mwanafunzi kutoka Madrassa AL-Sunnah – shule ya madrasa – mjini Mombasa. Picha/ Mishi Gongo

Mwalimu mwingine Ibrahim Pesa amewahimiza wazazi kutumia teknolojia kuwafundisha watoto wao.

“Ni wakati mgumu sana kwa wanafunzi. Walimu wa shule kupitia Wizara ya Elimu wameanzisha vipindi ambavyo vinawasaidia wanafunzi kusoma ili kuhakikisha kuwa wanajiendeleza na hawasahau walichofunzwa. Kwa watoto wa madrasa wazazi wanaweza kuwawekea watoto wao masomo kutoka kwa mitandao,” akaeleza.

Kupitia mitandao Ustadh Pesa alisema kuna masomo mbalimbali ambayo mwanafunzi anaweza kuangalia na akafuatilia.

“Kwa watoto wadogo kuna mafunzo yanayotolewa na vibonzo, miongoni mwa mafunzo hayo ni adabu za kula, jinsi ya kutawadha na kuswali, lugha ya mtoto anayopaswa kuzungumza na mzazi wake na watu wazima na hata Qur’an,” akasema.

Aidha alisema watoto wanafunzwa jinsi ya kujenga herufi za Kiarabu ili kuunda neno na mengine kadhalika.