Walimu wa shule miamba wa zamani wahepa wanahabari
JOSEPH WANGUI na GRACE GITAU
Walimu kutoka shule za upili ambazo kwa miaka mingi zilikuwa miamba wa elimu Jumapili hawakutaka kuhojiwa kuhusiana na matokeo ya shule zao, ishara kwamba huenda hazikufanya vyema katika mtihani wa KCSE mwaka huu.
Wakati huo huo, hakukuwa na mbwembwe na shughuli katika shule hizo ikilinganishwa na miaka ya awali ambapo walimu, wazazi na watahiniwa wangeimba na kufurahia alama nzuri za watahiniwa.
Kando na shule za kitaifa katika Kaunti ya Kiambu, shule nyingi zilizokuwa maarufu kwa matokeo mema katika Kaunti za Nyeri, Nyandarua, Kirinyaga na Murang’a hazikuwa miongoni mwa shule zilizotoa watahiniwa bora zaidi nchini.
Mwaka huu, Shule ya Upili ya Murang’a High ndiyo ilikuwa peke yake katika orodha ya 100 bora nchini.
Katika eneo hilo, Murang’a High iliongoza na alama za wastani 8.45 na kufuatwa na Pioneer School.
Shule ya Upili ya Njiiri, Murang’a ilikuwa na alama za wastani za 8.3 ilhali Shule ya Wasichana ya Kahuhia ilipata 7.9.
Taifa Leo haikupata alama za Shule ya Upili ya Kagumo na Shule ya Wasichana ya Bishop Gatimu Ngandu, ambazo ni shule za kitaifa, baada ya walimu kuomba muda zaidi kukusanya matokeo yote na kuchanganua ili kutoa “alama za wastani zinazoweza kuaminika.”
Mwalimu Mkuu wa Kagumo Dkt Silas Mwirigi alisema shule hiyo ilikuwa ikitegemea matokeo iliyopata kupitia kwa simu, hivyo ilikuwa vigumu kujua ilivyofanya shule hiyo.
“Hatujafanya vibaya lakini kwa sasa hatuwezi kutoa alama za wastani zinazoweza kuaminika kabla ya kupata matokeo yote,” alisema.
Shule hizo zaidi ya kuwa maarufu kwa matokeo mazuri, huwa zinatoa wanafunzi waliofanya vyema zaidi nchini.
Mwaka jana, Kagumo ilikuwa katika orodha ya shule zilizotoa watahiniwa bora zaidi nchini.
Shule ya Wasichana ya Bishop Gatimu Ngandu ilitoa wanafunzi wanne waliokuwa na alama A ilhali Shule ya Upili ya Kagumo ilikuwa na mwanafunzi mmoja aliyekuwa na A-.
Shule ya Upili ya Wasichana ya Mahiga, Othaya, iliongoza katika Kaunti ya Nyeri na alama ya wastani ya 8.138 kutoka 8.0, 2017.
Ingawa shule hiyo sio maarufu sana, ilishinda shule maarufu eneo hilo ikiwemo Bishop Gatimu Ngandu. Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Fransisca Wahome na mwenyekiti Wahome Gikonyo walisema shule hiyo ilifanya vyema kutokana na juhudi za pamoja miongoni mwa wazazi, walimu na wanafunzi.
“Tulikuwa na lengo la kupata tisa, alama za wastani, lakini mwaka ujao, tutajikakamua kupata kwa kusuluhisha baadhi ya changamoto,” alisema Bw Wahome.
Shule hiyo ilikuwa na watahiniwa 203 ambao walimaliza silabasi mnamo Februari, alisema Bi Wahome.