Habari Mseto

Walimu wakuu Khwisero walalamikia kuongezeka visa vya wizi wa mabavu

July 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SHABAN MAKOKHA

[email protected]

WALIMU WAKUU katika kaunti ndogo ya Khwisero katika Kaunti ya Kakamega wanalalamika kuhusu kuongezeka kwa visa vya kusikitisha vya wizi wa kimabavu unaotekelezwa katika shule za eneo hilo.

Walimu hao waliokuwa wakiongea Ijumaa wakati wa uzinduzi wa mkakati wa kuboresha usimamizi shuleni, walisema visa vya watu wasiojulikana kuvamia na kuiba vitu na kuharibu mali shuleni vimeongezeka.

Ripoti zinasema zaidi ya shule 15 za msingi na sekondari zimevamiwa ambapo mali ambayo thamani yake haijulikani imeibwa.

Mwalimu wa shule ya upili ya Mwihila, Bw Musonye Namusende alisema wezi hao kando na kuiba vifaa vya masomo pia wanaiba chakula.

“Tuna wasiwasi kuhusu hali ya usalama katika shule za Khwisero kwa sababu wezi wanaiba vifaa vya kutumika katika masomo mbalimbali na vilevile chakula,” alisema Bw Namusende.

Mwalimu huyo alitaja vipakatalishi kuwa ni miongoni mwa vifaa ambavyo vimeibiwa.

Baadhi ya shule ambazo zimeathirika ni Emalindi Girls, Mwihila Girls, Ematundu Secondary, Ebuyonga Primary, Emulole Primary na Emalindi Primary.

Ni hali ambayo walimu wengi wana wasiwasi kuhusu usalama wa wanafunzi, hasa wasichana.

Afisa wa Elimu katika kaunti ndogo ya Khwisero, Bi Gentrix Amatsa alithibitisha wezi waliiba mahindi na maharagwe ya kutumika kwa mpango wa chakula shuleni na pia vifaa vya kielektroniki vya elimu kidijitali katika Shule ya Msingi ya Ebuyonga.

Pia alisema vifaa vya kidijitali vilipotea kwa njia ya wizi katika Shule ya Msingi ya Emulole.

“Shuleni Emulole wezi waliiba vifaa vya kielektroniki vilivyotolewa na serikali kuu katika mpango wa kuimarisha elimu kwa mfumo wa kidijitali (DLP),” alisema Bi Amatsa ambaye amewataka walimu wakuu wawe macho zaidi kuona wanakabiliana na changamoto za kiusalama.

Kamanda wa polisi katika eneo hilo, Miriam Omonyi amesema hawajashika wezi hao kwa sababu “ripoti tulizopata zingali za mwanzo kabisa bila kutoa fununu za maana.”

“Kwa sasa hatuna idadi kamili ya vifaa na kiwango cha chakula kilichoibiwa. Hata hivyo, tunawawinda wezi hao na tutajua nia yao ni gani,” akasema Bi Omonyi.

Hata hivyo, afisa huyo amesema huenda kuna njama za kuhujumiana kisiasa kwa sababu uchunguzi husishi ambao amekuwa akifanya “unaonyesha baadhi ya watu hawafurahishwi na mpango wa chakula shuleni ulioanzishwa na mbunge wa eneo hilo, Bw Christopher Aseka.