Habari Mseto

Walimu watoa masharti ya shule kufunguliwa

October 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

WALIMU Jumatatu walitoa orodha ya mambo ambayo wanataka serikali itekeleze kabla ya kufungua shule.

Vyama vya Knut na Kuppet vilisema kuwa serikali ni sharti iweke mikakati ya kuhakikisha kuwa walimu hawataambukizwa virusi vya corona shule zitakapofunguliwa.

Katibu Mkuu wa Knut, Wilson Sossion aliitaka serikali kuwahakikishia walimu kuwa watapata matibabu ya bure au gharama nafuu iwapo wataambukizwa virusi vya corona wakiwa shuleni.

Walimu wanataka pia kushirikishwa katika maandalizi ya kalenda ya elimu na mwongozo kuhusu jinsi ya kufidia muda ambao watoto walipoteza shule zilipofungwa kwa sababu ya janga la virusi vya corona.

“Serikali inafaa kutoa taarifa za mara kwa mara kwa wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine shuleni ili kuwaondolea hofu ambayo imesababishwa na janga la virusi vya corona,” akasema Bw Sossion.

Chama cha Knut pia kinataka serikali kujenga madarasa zaidi ili kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.

“Kuongezwa kwa madarasa kunamaanisha kuwa shule za umma zitahitaji walimu zaidi. Hivyo, Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) ni sharti itengewe fedha za kutosha kuajiri walimu zaidi,” akasema Bw Sossion.

Wito sawa huo pia ulitolewa na Katibu Mkuu wa Kuppet Akelo Misori ambaye alisema kuna uhaba wa walimu 150,000 katika shule za umma.

Bw Misori aliyekuwa alisema kuwa janga la virusi vya corona limeongeza tatizo la uhaba wa walimu.

Bw Sossion aliongeza kuwa walimu wanahitaji kupewa ushauri nasaha kabla ya kufunguliwa kwa shule.

“Walimu wengi waliathiriwa kisaikolojia na janga la virusi vya corona. Hivyo wanahitaji kupewa huduma za ushauri nasaha kabla ya kuanza kufundisha,” akasema mbunge huyo maalumu wa ODM.

Mafunzo 

Chama cha Knut pia kinataka serikali kuwapa mafunzo spesheli walimu ambao wana zaidi ya umri wa miaka 58 na wale walio na maradhi kama vile Ukimwi, kisukari na presha ya damu ili kuwalinda dhidi ya kupatwa na virusi vya corona.

Chama cha Knut kimekosoa Wizara ya Elimu kwa kuagiza walimu kwenda shuleni bila kuwaeleza mambo wanayostahili kufanya.

“Sasa ni wiki ya pili baada ya TSC kuagiza walimu kwenda shuleni. Lakini kufikia sasa hawana kazi ya kufanya. Wizara ya Elimu inafaa kutoa kalenda ya elimu ili walimu waitumie kufanya maandalizi,” akasema.

Wakati huo huo, Serikali jana iliendelea kunyamazia masuala kuhusu tarehe ya kufunguliwa kwa shule, wanachopasa kufanya walimu waliorejea shuleni pamoja na fedha za maandalizi ya kukabili virusi vya corona shule zikifunguliwa.

Waziri wa Elimu George Magoha akiwa Nyeri Jumatatu alikataa kujibu maswali ya wanahabari kuhusu masuala hayo.

Habari za ziada na Regina Kinogu