Habari Mseto

Walioathiriwa na mafuriko sasa walemewa na matatizo ya akili

June 13th, 2024 2 min read

SAMMY LUTTA NA BARNABAS BII

MAMIA ya familia zilizohamishwa na mafuriko katika ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa zinakabiliwa na hatari ya kupatwa na matatizo ya afya ya akili.

Hii ni baada ya kupatwa na matukio mengi ambayo yalisababisha mauti ya raia na uharibifu wa mali uliotokea kwao.

Baadhi ya familia katika Kaunti ya Turkana zinahitaji huduma za ushauri na nasaha kutokana na kulemewa na athari za janga hilo la mafuriko.

Kwa mujibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya, mafuriko hayo yalisambaratisha njia ya mapato ya wengi na pia kuharibu nyumba zao, na kwa sasa wanahangaika kurejea katika makazi yao.

“Familia ambazo zilihamishwa na maji ya mafuriko zinahitaji huduma za ushauri na nasaha. Pia zinahitaji kupewa huduma za kimatibabu ili kuyazuia magonjwa ya kuambukizana,” akasema Oscar Okumu, Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu kutoka ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Bw Okumu alisema kamati kuhusu udhibiti wa majanga eneo hilo imeanza kukumbatia mipango ya kuziokoa familia ambazo ziliathirika na mafuriko.

Kamati hiyo inapambania kuzuia magonjwa, kudhibiti majanga na kukumbatia mipango ya kuwasaidia walioathirika kurejelea maisha yao kama kawaida.

Pia shirika la msalaba mwekundu linatathmini hasara ambayo ilisababishwa na mafuriko katika Kaunti za Turkana, Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet, Trans Nzoia, Uasin Gishu, Nandi na Bungoma.

“Tumesambaza vyakula na bidhaa nyingine lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya kudhibiti magonjwa na pia kushughulikia afya ya kiakili ya familia ambazo ziliathirika na mafuriko,” akaongeza Bw Okumu.

Afisa huyo alisema kuwa Turkana ya Kati iliathirika sana na mafuriko hayo na mipango ambayo imekumbatiwa itazisaidia familia kujikwamua kutokana na athari za mafuriko.

Inakadiriwa kuwa watu 291 walipoteza maisha yao, 188 wakajeruhiwa na familia 90,000 kuhama makwao kutokana na mafuriko hayo. Zaidi ya watu 72 nao waliripotiwa kutoweka kati ya Machi na Mei.

Mimea ambayo ilikuwa katika ekari kadhaa za ardhi nayo ilisombwa na mengine kufunikwa na maji Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Eneo hilo ndilo ghala la taifa na njaa inanukia nchini kutokana na athari ya mafuriko hayo.

Kando na hayo, mafuriko yalisababisha kuharibiwa kwa miundomsingi ikiwemo barabara na mali ya kaunti.

Mamia ya wafanyabiashara na wakulima eneo hilo nao walipata hasara ya mamilioni ya pesa baada ya biashara zao, mifugo na mimea kuharibiwa au kusombwa na maji ya mafuriko.

Katika Kaunti ya Pokot Magharibi, mimea mingi ilisombwa na maji ya mafuriko na pia kulikuwa na maporomoko ya ardhi.

Kondoo 300 waliaga baada ya maparomoko ya ardhi kutokea katika kijiji cha Chepkaram, Tapach. Kaunti ndogo ya Pokot Kusini.

Kaunti za Nandi, Pokot Magharibi, Nandi, Mlima Elgon pia ziliathirika na maporomoko ya ardhi.