Habari Mseto

Waliofungwa maisha kwa kumficha gaidi wa Al Qaeda waomba korti iwahurumie

March 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA PHILIP MUYANGA

Mwanamume mwenye umri wa miaka 59, pamoja na mwanawe wa kiume waliofungwa kifungo cha maisha gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kumhifadhi aliyekuwa mshirika mkuu wa kundi la kigaidi la Al Qaeda Fazul Abdullah, wamekata rufaa katika Mahakama Kuu.

Bw Mahfudh Ashur Hemed na mwanawe Ibrahim Mahfudh Ashur katika stakabadhi zao za rufaa wanataka mahakama kufutilia uamuzi huo wa mahakama ya chini na kuamuru waachiliwe huru.

Kupitia mawakili wao,wanasema kuwa hakimu alikosea kisheria kuendelea na kesi hiyo hadi akaiamua kwa kutumia shtaka ambalo lilikuwa na makosa.

“Hakimu alikosea kisheria kwa kuhukumu licha ya upande wa mashtaka kutothibitisha kukikamilifu masuala muhimu katika shtaka,” stakabadhi za kesi zilisema.

Katika rufaa walisema kuwa hakimu alikosea kisheria kwa kusema kuwa Fazul alikuwa katika nyumba ya Bw Mahfudh.

Waliongeza kusema kuwa hakimu alikosea kisheria kwa kumhukumu na kumfunga Bw Ibrahim kwa sababu ya kuamini na sio ushahidi uliotolewa katika kesi hiyo ambayo ilichukua zaidi ya miaka 11.