Habari Mseto

Waliokwepa kulipa ushuru wa Sh50 milioni waitwa kortini

September 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

WAFANYABIASHARA wanne Jumanne waliagizwa wafike kortini Septemba 27 kujibu mashtaka ya kukwepa kulipa ushuru wa Sh50 milioni.

Hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Nairobi Bw Francis Andayi aliwamuru Mabw Bhupen Vichand Gala, Ahmmed Mohammed Osman, Simeon Nyadema Mokaya na Bi Esther Moraa Mwambi wajisalamishe mahakamani kujibu mashtaka waliyofunguliwa na Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA).

Afisa anayeongoza mashtaka katika kesi za kukwepa ushuru Bi Irene Muthee alimweleza hakimu kuwa wafanyabiashara hao waliarifiwa wafike kortini jana kujibu mashtaka lakini wakakaidi agizo.

“Naomba hii mahakama itoe kibali cha kuwashurutisha Mabw Gala, Osman , Mokaya na Bi Mwambi kufika kortini kujibu mashtaka ya kukwepa kulipa ushuru wa thamani ya ziada VAT,” Bi Muthee alisema.

Bi Muthee aliomba korti iamuru maafisa wa korti wawapelekee samanzi washtakiwa wakiagizwa wafike kortini kujibu mashtaka,

“Naomba korti iamuru washtakiwa wafike kortini kujibu mashtaka ambayo walIkuwa wamearifiwa hapo awali,” alidokeza Bi Muthee.

Alieleza kuwa washtakiwa hao wamekwepa kufika mahakamani ilhali walikuwa wamejulishwa.

Bi Muthee aliomba apewe muda wa mwezi mmoja kuwafikisha washtakiwa kortini lakini hakimu akamweleza mwezi mmoja ni muda mwingi sana.

“Mwezi mmoja ukiwasaka washtakiwa ni muda mrefu ikitiliwa maanani unajua mahala unaweza kuwapata. Kesi hii itatajwa tena Septemba 27 wajibu mashtaka dhidi yao,” aliamuru Bw Andayi.

Bw Gala , ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Kentsa Metal & Hardware Limited  anakabiliwa na shtaka la kukataa kulipa ushuru wa VAT wa  Sh26,621,293.

Bi Muthee  pia alimshtaki Bw Gala kwa kutoa taarifa ya kupotosha kwa maafisa wa KRA kuhusu malipo ya ushuru ya kampuni yake na kuisbabisha isilipe kitita cha Sh na kusababisha kampuni hiyo isilipe kodi ya Sh5,128,263.

Bw  Andayi alifahamishwa Bw Mokaya  na Bi Mwambi , wakiwa wakurugenzi wa makampuni ya

Botana Kenya Limited na Kihunya Construction Limited walikosa kulipa ushuru wa VAT wa kima cha zaidi ya Sh11milioni kati ya Januari 2011 na 2013.

Mashtaka yalisema kuwa washtakiwa hao waliinyima nchi hii kodi ya mapato na kuathiri kifedha.

Bw Osman anakabiliwa na shtaka la kuficha aliigiza humu nchini tairi 725 ambazo zingelilipiwa ushuru wa Sh784,838.

Fomu alizowasilisha kwa KRA zilionyesha aliigiza tairi  hizo lakini hakulipa ushuru wa mapato.

Mahakama iliambiwa Bw Osman hakulipa ushuru huo kati ya 2011 na 2018.