Walionaswa na kilo 4.6 za dhahabu watupwa rumande siku 10
Na RICHARD MUNGUTI
WASHUKIWA wawili ambao uraia wao haujajulikana waliokamatwa katika kizuizi cha barabara ya Isiolo-Moyale wakiwa na takriban kilo 4.6 za dhahabu na pesa za kigeni Euro 50,150 ( KSh5,666,950) wameagizwa wakae rumande kwa muda wa siku kumi.
Hakimu mkazi Bi Zainabu Abdul alikubalia ombi la polisi washukiwa hao Issa Mohammed Dubow na Yunis Maalum Muktar wazuiliwe wahojiwe na uraia wao ujulikane.
Bi Abdul alielezwa na Sajini Stanley Musembi kuwa polisi wanashuku wawili hao wanahusika na uhalifu wa kimataifa na itabidi “kitengo cha Polisi cha Interpol kishirikishwe.”
“Maafisa wa polisi wa kitengo cha uhalifu wa kimataifa watabaini ikiwa wawili hawa ni miongoni mwa washukiwa ambao majina yao yamechapishwa katika mitandao ya kimataifa kuhusika na biashara ya magendo ya dhahabu na ulanguzi wa pesa,” Sgt Musembi alidokeza.
Katika taarifa ya kiapo aliyowasilisha mahakamani na Sgt Musembi, simu za kiunga mbali cha washukiwa hao ziko na habari muhimu kuhusu biashara zao.
“Simu za washukiwa hawa wawili zapasa kupelekwa katika kitengo cha polisi wa kupambana na uhalifu wa kimitandao zichunguzwe wanaoshirikiana nao katika biashara hii haramu,” Bi Abdul alifahamishwa.
Washtakiwa hawa walikamatwa katika kituo cha kukagua magari katika barabara ya Thika-Kitui ikiwa na dhahabu na pesa hizo za kigeni mnamo Machi 18, 2019.
“Washukiwa walikamatwa katika kizuizi cha barabara katika eneo la Kalama kwenye barabara ya Isiolo-Moyale wakiwa na dhahabu na pesa za kigeni,” alisema Sgt Musembi.
Aliomba akubaliwe apeleke madini hayo kwa Kitengo cha Kupima cha Madini na Jiolojia kubaini ikiwa ni dhahabu au ni madini mengine.
Mahakama ilifahamishwa maafisa wa polisi kutoka kitengo cha Interpol na wale kutoka kitengo cha uhalifu wa kimataifa watafanya juhudi za pamoja kukamilisha uchunguzi huo katika muda wa siku 10.
Pia hakimu alisema wakati wa mahojiano washukiwa wataeleza polisi waliko washukiwa wengine wanaoshirikiana nao katika biashara hiyo haramu.
Korti ilijulishwa washukiwa hao watafunguliwa mashtaka ya ulanguzi wa pesa na kufanya biashara ya magendo ya dhahabu.