• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Waliotafuna mamilioni ya corona kujua hatima yao baada ya siku 14

Waliotafuna mamilioni ya corona kujua hatima yao baada ya siku 14

Na CHARLES WASONGA

WAHUSIKA katika sakata ya ununuzi wa vifaa vya Covid-19 katika Mamlaka ya Ununuzi wa Dawa na Vifaa vya Kimatibabu (KEMSA) na kupelekea matumizi ya Sh7.8 bilioni kinyume cha sheria sasa watajua ikiwa watashtakiwa au la baada ya siku 14.

Hii ni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kutangaza kuwa amepokea faili ya uchunguzi wa sakata hiyo kutoka kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ambayo.

Kwenye taarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari ijumaa, Septemba 18, jioni Bw Haji alisema ameteua kundi la waendesha mashtaka wenye tajriba pevu kuchambua faili hizo na kuwasilisha ripoti kwake ilia atoe mwelekeo kuhusu suala hilo.

“Leo, Septemba 18, 2020 nimepokea faili ya uchunguzi kutoka kw EACC kuhusu ununuzi wa vifaa vya Covid-19, ulioendeshwa kinyume cha sheria na malipo ya Sh7.8 bilioni kwa wawasilishaji bidhaa hizo. Afisi yangu itachunguza faili hizo kisha kutoa mwelekeo,” akasema Bw Haji.

Mnamo Agosti 15, 2020 bodi wa wasimamizi ya Kemsa inayoongozwa na aliyekuwa Seneta wa Murang’a Kembi Gitura iliwasimamisha kazi kwa muda, Afisi Mkuu Mtendaji John Manjari, Mkurugenzi wa Ununuzi Charles Juma na Mkurugenzi wa Masuala ya Biashara Eliud Muriithi ili kutoa nafasi kwa EACC kuchunguza sakata hiyo.

Ilidaiwa kuwa jumla ya kampuni 60, zingine ghushi , zilipewa zabuni ya kuwasilisha vifaa vya kujikinga dhidi ya virusi vya corona (PPEs), Maski na bidhaa nyinginezo kwa bei ya juu kupita kiasi, hali iliyopelekea kupotea kwa fedha za umma.

Watu kadhaa wamehojiwa kuhusiana na sakata hiyo akiwemo Naibu mwenyekiti wa Jubilee David Murathe ambaye alidaiwa kuwa na uhusiano na kampuni kwa jina Kiling Ltd iliyopewa zabuni ya thamani ya Sh4 bilioni.

Makataa ya siku 30 ambayo Rais Uhuru Kenyatta alikuwa ametoa kwa asasi za uchunguzi kukamilisha uchunguzi kuhusu sakata hiyo ilikamilisha mnamo Jumatano wiki hii. Sakata hiyo pia inachunguzwa na Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Afya na Kamati ya Seneti kuhusu Afya. Miongoni mwa wale ambao wamehojiwa na Kamati hizi ni Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, Katibu wake Susan Mochache na maafisa hao watatu wa Kemsa na wanachama wa bodi ya mamlaka hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Kisumu All Stars kutaja benchi mpya ya kiufundi

Familia 1,000 zaachwa bila makao Turkana