Waliovuta bangi ili wakanengue viuno kwa shoo ya Freddie McGregor wajikanganya mahakamani
Na RICHARD MUNGUTI
WANASARAKASI wawili walijikanganya mahakamani waliposhauriwa na hakimu wakiri mashtaka ya kupatikana na bangi misokoto mitano kisha waombe msamaha wasamehewe ili waachiliwe waende nyumbani.
“Najua kwamba mlikuwa mnaivuta hii bhangi ndipo mkacheze densi katika tafrija iliyoandaliwa na mchezaji regge wa kimataifa Bw Freddie McGregor aliyekuwa ameandaa shoo katika ukumbi wa Jomo Kenyatta International Conference (KICC),” hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi aliwaambia wawili hao.
“Si ni kweli mlikuwa mnavuta ili mkacheze densi?” Bw Andayi aliwauliza wawili hao waliOkuwa na mtindo wa nywele wa Rasta.
“Ni kweli . Tulikuwa tumewasha msokoto wa kwanza polisi walipotufumania,” alijibu Munene
“Milikuwa mmepatikana na misokoto hii ni kweli au sio kweli?” hakimu aliwahoji zaidi.
“Hapana huyu mwenzangu ndiye alinipa msokoto wa kwanza kuvuta. Sikuwa na bangi hii mimi,” alijibu Kamau.
Hakimu akasema, “Badala ya kuenda jela zaidi ya miaka saba nawashauri ombeni msamaha mkisema kwamba ni upumbavu mko nao wa ujana na kwamba hamtarudia tena kupatikana na bangi ndipo niwaachilie mkashiriki katika ujenzi wa taifa.”
‘Siwezi kujiita mpumbavu’
“Mimi siwezi kusema ni mpumbavu hata!,” akasema Kamau.
“Wacha nikushauri usijaribu kuwa mwerevu. Mtaumia bure tu na kukaa rumande kabla ya kesi inayowasubiri kusikizwa na kuamuliwa,” hakimu aliwashauri .
Hakimu aliwashauri adhabu ya msokoto mmoja na tani za mhadharati huu uliopigwa marufuku ni moja tu.
Kamau aling’ang’ana kujinasua na kutopatikana na bangi hiyo ndipo hakimu akawaambia, “kwa vile mmekataa kusikiza ushauri sasa mtaenda rumande na kila mmoja wenu ataachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000 ama dhamana ya pesa taslimu Sh50,000.”
Munene, kusikia mambo yamewaendea mrama alirudi tena kizimbani na kumsihi hakimu amsamehe lakini akaambiwa , “ mmepewa fursa mjiokoe lakini mkakataa.”
“Naomba niachiliwe nikalipe nyumba kwa vile itafungwa na Landilodi,” alimweleza hakimu huku akiambiwa , “Tuma pesa kwa njia ya mtandao wa Mpesa kwa landlilodi wako.”
“Haki ya Mungu niko na Sh500 tu kwa mfuko,” Munene alimweleza hakimu huku akiomba msaada lakini akajibiwa , Mngikubali ushauri mngekuwa nje sasa lakini sasa lipeni dhamana mtoke.”
Shtaka dhidi yao lilisema walikutwa na misokoto mitano ya bhangi Machi 4 katika uwanja wa KICC.