Waluke adai kuwalipia dhamana mahabusu 57
Na BRIAN OJAMAA
MBUNGE wa Sirisia, Bw John Waluke aliyeachiliwa huru kwa dhamana wiki mbili zilizopita kutokana na sakata ya wizi wa fedha za mahindi, sasa anadai kuwa aliwalipia dhamana wafungwa 57 kabla ya kuondoka gerezani.
Mbunge huyo ambaye alikuwa akizuiliwa gerezani kwa karibu miezi minne, alisema kuwa alilipia wafungwa dhamana ya kati ya Sh1,000 na Sh10,000.
“Kuna mamia ya watu ambao wanazuiliwa rumande kwa zaidi ya mwaka mmoja kwa kushindwa kulipa dhamana ya Sh1,000. Niliamua kuwalipia ili waende nyumbani kesi zao zikiendelea kusikizwa. Nilifanya hivyo kwa nia njema kama mbunge,” akasema Bw Waluke.
Mbunge huyo alihukumiwa kifungo cha miaka 74 baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika katika ufisadi.
Kampuni yake Erad Supplies inadaiwa kupokea Sh297 milioni za bwerere kutoka kwa serikali.
“Maisha ya gerezani ni magumu sana. Watu wanahangaika na watu wote wanashughulikiwa sawa bila kujali cheo,” akasema.
Bw Waluke alisema kuwa, “ Wafungwa wanalishwa kama wanyama. Wafungwa wanakula chakula cha mchana saa kumi alfajiri asubuhi na maakuli ya mchana saa mbili asubuhi. Wafungwa hutumia muda mrefu wakiwa ndani ya gereza.”
“Ndani ya gereza kuna ‘gavana’ (kiranja) ambaye pia ni mfungwa. Kazi ya gavana ni kutuelekeza, kujigeuza usiku tunapolala,” akaelezea.
Bw Waluke pamoja na mshtakiwa mwenzake Grace Wakhungu walienda kortini wakitaka waachiliwe huru kwa dhamana hadi pale mahakama itasikiliza na kuamua rufaa yao.