Habari Mseto

Waluke, Wakhungu kujua hatima yao Sept 25

August 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MBUNGE wa Sirisia John Waluke na Grace Wakhungu wanaotumikia vifungo vya miaka 62 na 67 mtawalia watajua hatma yao Septemba 25, 2020 Mahakama kuu itakapoamua ikiwa wataachiliwa kwa dhamana.

Waluke na Wakhungu waliohukumiwa Juni 26, 2020 waliomba mahakama kuu iwaachilie kwa dhamana kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa rufaa walizokata kupinga vifungo vikali walivyohukumiwa kwa ulaghai wa Sh313 milioni walizopokea kutoka kwa halmashauri ya nafaka na mazao (NCPB).

Walipokea pesa hizo wakidai walikuwa wamenununua kutoka ng’ambo tani 40,000 za mahindi.

Hakimu mkuu Bi Elizabeth Juma aliwapata wawili hao kwa hatia ya kupokea pesa kwa njia ya ungandanyivu na kuwatoza faini ya Sh1bilioni kila mmoja.

Mawakili Samson Nyaberi na Paul Muite waliowasilisha maombi ya wafungwa hao kuachiliwa kwa dhamana walieleza mahakama wawili hao wako na changamoto za magonjwa na kumsihi Jaji John Onyiengo atilie maanani hali yao na umri wao na kuwaachilia kwa dhamana.

Grace Wakhungu yuko na umri wa miaka 80 ilhali Waluke yuko na umri wa miaka zaidi ya 60.

“Hali ngumu ya gerezani haichukuani vyema na umri wa wafungwa hawa walio na changamoto za kiafya. Naomba hii mahakama itilie maanani ugonjwa Corona unaoathiri walio na umri mkubwa na kuwaachilia wafungwa hawa kwa dhamana,” Bw Muite alisema.

Jaji Onyiengo alielezwa rufaa walizokata wafungwa hao zitafaulu kwa vile kulikuwa na kasoro tele katika ushahidi uliotolewa.

Pia mawakili walisema kiwango cha faini waliyotozwa kilikuwa juu mno na hakimu hakuzingatia vipengee muhimu vya sheria kabla ya kuwatoza faini hiyo.

Hakimu alisema Waluke alikiri alipokea Sh50milioni naye Grace akapokea Sh40milioni kati ya Sh313milioni zilizolipwa kampuni yao Erad Supplies & General contracts ltd na NCPB.

Lakini mahakama kuu iliruhusu Daktari wa kibinafsi amtembelee Wakhungu katika gereza la Lang’ata kupokea matibabu.

Ombi la kuachiliwa kwa dhamana lilipingwa vikali na naibu wa mkurugenzi mkuu wa mashtaka Alexander Muteti akisema hakimu alipitisha adhabu iliyostahili.