Habari Mseto

Wamakonde wahofia kupoteza uraia wa Kenya huku Msumbiji ikiwanyemelea

February 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MKAMBURI MWAWASI

JAMII ya Wamakonde inahofia kupoteza uraia wake wa Kenya baada ya madai ya kuwepo shughuli ya usajili mpya wa jamii hiyo na maafisa wa taifa la Msumbiji.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa jamii hiyo Kaunti ya Kwale Bw Thomas Nguli, maafisa kutoka ubalozi wa Msumbiji wamekuwa wakishinikiza usajili wa jamii hiyo inayosisitiza kuwa raia wa Kenya.

Katika kikao na wanahabari, Nguli amemtaka Waziri wa Usalama nchini Prof Kithure Kindiki kuingilia kati ili kusitisha shughuli hiyo mara moja.

“Watu wetu walikuwa wametelekezwa na serikali ya Kenya ikachukua jukumu la kutuandikisha kuwa Wakenya na hata kupata vitambulisho,” alisema Bw Nguli.

Bw Nguli aliongeza kwamba Msumbiji imeingiza siasa katika suala hilo ili kuwaandikisha Wamakonde upya baada ya kupata vyeti vya humu nchini.

“Serikali ya Msumbiji inaangalia maslahi yake ya kupata kura kutoka kwa Wamakonde walioko nchini Kenya. Wamekuwa wapi miaka yote tukiteseka bila vyeti?” aliuliza Bw Nguli.

Wakati uo huo, mwenyekiti huyo amekiri kuwa jamii hiyo imefaidika pakubwa tangu ipate vitambulisho vya kitaifa na serikali ya Kenya miaka saba iliyopita.

Ubaguzi

“Kama kiongozi, nilipigania uraia na hatukuwa na stakabadhi za humu nchini ili kupata huduma kama watu wengine na wala hatukuruhusiwa kuwa na uraia mara mbili,” alisema Bw Nguli.

Bw Nguli aliwaomba Wamakonde wote wasikubali kutumiwa vibaya kwa sababu ya masuala ya siasa akiongeza kwamba si Wamakonde wote wanatoka Msumbiji.

Zaidi ya watu elfu tatu kutoka jamii hiyo inayoishi Kwale ambayo chimbuko lake ni Mozambique wamesajiliwa kuwa Wakenya.

Jamii ya Wamakonde ilikuwa miongoni mwa watu wengine wasio na utaifa ambao wamekuwa wanaishi katika eneo la Pwani kwa miongo kadhaa baada ya wazazi wao kuja nchini kabla ya uhuru kama vibarua wa mkonge na sukari katika mashamba ya Kilifi, Kwale na Taita Taveta.

Mnamo Desemba 2016, baada ya miaka mingi ya kutaka kutambuliwa kama Wakenya, Wamakonde walitunukiwa rasmi uraia wa Kenya.

Aliyekuwa Rais wakati huo Uhuru Kenyatta aliwatambulisha Wamakonde kuwa kabila la 43 la Kenya mnamo Februari 2017.