Wamiliki baa wataka Gachagua aombe ushauri wao kumaliza pombe ya mauti
NA KEVIN CHERUIYOT
CHAMA cha Kitaifa cha Wamiliki wa Baa (BAHLITA), kimefichua kwamba kinawafahamu watu ambao wamekuwa wakieneza pombe haramu inayolaumiwa kwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu 20 katika Kaunti ya Kirinyaga.
Hata hivyo, chama kilisema kuwa watu wanaoeneza vileo hivyo hatari wamemzingira Naibu Rais Rigathi Gachagua, ambaye amekuwa akiongoza vita dhidi ya pombe hizo.
Kilisema kuwa juhudi zake kuiambia Serikali ya Kitaifa kuhusu jambo hilo zimegonga mwamba.
Kwa sasa, chama hicho kinamrai Bw Gachagua kukishirikisha kwenye juhudi hizo, kikisema kuwa kuna maelezo ya kijasusi kuhusu vile kemikali haramu aina ya ethanol imekuwa ikiingizwa nchini kutoka nje kwa njia ya kimagendo.
Mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho, Bw Simon Njoroge, alisema kuwa kufunga baa na vilabu hakutakuwa suluhisho, kwani pombe hiyo itasambazwa katika maeneo mengine nchini, na madhara yatakuwa yale yale yaliyoshuhudiwa katika Kaunti ya Kirinyaga.
“Kama chama, tunajua yule anayetengeneza pombe hizo na wale wanaozisambaza. Huwa zinasambazwa nyakati za mchana. Ni wakati serikali itangaze kujitolea kwake, kwani kama chama, tumejitolea kikamilifu,” akasema Bw Njoroge.
Alisema kuwa vita dhidi ya pombe hizo nchini vinafaa kuendeshwa na kila mdau, zikiwemo serikali za kaunti, kwani ndizo zimekuwa zikitoa leseni.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw Boniface Gachoka, alisema kuwa baadhi ya wanasiasa katika chama tawala wamekuwa wakitumia ushawishi wao kuwazuia kuwasilisha malalamishi yao kwa Bw Gachagua.
“Kuna watu walio karibu na Naibu Rais, tunaohisi kwamba wametuzuia kumwona…sisi ndio tuna maelezo ya kijasusi. Kuna makateli, mabwanyenye walio serikalini, ilhali wao ndio wanaotoa vitisho kwa maafisa wanaoendesha juhudi za kukabili pombe hizo na wanachama wetu kutotoa siri hizo,” akasema Bw Gachoka.