Habari Mseto

Wanabodaboda wonywa dhidi ya kutongoza wasichana wa shule

May 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

WAHUDUMU wa bodaboda wameonywa vikali dhidi ya kutongoza wasichana wa shule.

Afisa mkuu wa polisi Thika Magharibi, Bi Beatrice Kiraguri, alisema imebainika wazi kuwa wengi wa wahudumu wa bodaboda hupenda kuwazuzua kimapenzi wanafunzi wa shule wanapowabeba kwenye pikipiki zao.

“Tumepata ripoti hizo kuwa nyinyi hupenda kuwahadaa wanafunzi hao wakati wanapoabiri pikipiki zenu. Nini huwa mnaona kwa wasichana hawa? Ni vyema muwe mfano mwema kwa umma,” alisema Bi Kiraguri

Aliyasema hayo wakati wahudumu wa bodaboda walipokuwa wakihamasishwa kuhusu sheria za barabara katika uwanja wa Community, mjini Thika.

Afisa mkuu wa trafiki Bi Elenah Wamuyu, aliwataka wahudumu wa bodaboda kufuata sheria zote za barabara kwa kujihami na vifaa vyote vinavyohitajika.

Wahudumu hao wa bodaboda walihimizwa kuhudhuria shule ya kuendesha pikipiki ili kupata leseni, kuvalia jezi rasmi na helmeti.

“Iwapo kila mmoja wenu atafuata sheria inavyostahili bila shaka hakuna yeyote atahangaishwa na polisi,” alisema Bi Wamuyu.

Wanabodaboda walihimizwa kushirikiana na polisi ili kukabiliana na wahalifu ambao hutumia bodaboda kuibia wanawake vibeti.

Maafisa wa polisi wakiwahamasisha wanabodaboda kuhusu haja ya kuzingatia maadili kwa kazi yao. Picha/ Lawrence Ongaro

“Nyinyi wanabodaboda ndio mtaweza kutusaidia kupambana na wahalifu hawa ambao siku zao zimehesabiwa,” alisema Bi Wamuyu.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika, Bw Alfred Wanyoike aliwahimiza wazingatie biashara yao kwa uwazi bila kuingilia mambo maovu.

“Ni vyema kuendesha biashara yenu kwa njia ya haki na mhakikishe mnawatendea wateja wenu haki wakati wa kuendesha kazi hiyo,” alisema Bw Wanyoike.

Alisema mbunge wa Thika Mhandisi Patrick Wainaina ametenga Sh500,000 zitakazotumika kuwafadhili wanabodaboda kuhudhuria masomo ya kuendesha pikipiki ili wawe na ujuzi kamili.

“Kwa hivyo itabidi muende shule ili muwe wajuzi wa kuendesha pikipiki kwa njia ifaayo,” alisema Bw Wanyoike

Wahudumu hao kwa kauli moja walikubaliana na pendekezo hilo na kwa sauti moja waliapa mbele ya umati ya kwamba watakuwa mstari wa mbele kukabiliana na wahalifu hao.

Mkutano huo ulihudhuriwa na washikadau wote wa kibiashara na wakazi wa Thika ambao pia walisema watashirikiana na polisi ili kupambana na wahalifu.

Wanabodaboda hao kwa kauli moja waliapa ya kwamba wanazidi kushirikiana na  maafisa wa polisi na kuhakikisha wanawatendea haki wateja wao .

Wanabodaboda wa Thika walitoa malalamiko yao wakisema ya kwamba kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakihangaishwa na polisi wawili wa trafiki na wangetaka maafisa hao waondolewe Thika wapelekwe kwingine.

Agizo hilo lilitiliwa maanani na afisa mkuu wa Polisi Bi Kiraguri akisema hatua ya haraka itachukuliwa mara moja.