• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Wanachama Thingira Car Wash wanufaika kwa kupokezwa sare za kazi

Wanachama Thingira Car Wash wanufaika kwa kupokezwa sare za kazi

Na LAWRENCE ONGARO

KIKUNDI kinachowaleta pamoja watu 30 wanaojihusisha na uoshaji wa magari wamenufaika pakubwa baada ya kupokea sare rasmi za kazi.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alilazimika kufanya juhudi ya kuwafaidi na sare hizo baada ya wao kusumbuliwa na polisi kwa muda mrefu.

Kikundi hicho kinajulikana kama Thingira Car Wash na liko mjini Thika.

Mwenyekiti wao Bw Julius Mucheru alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakiendesha kazi hiyo bila kuwa na sare maalum na kwa hivyo wakati wowote polisi walipofukuza wahalifu waliopitia mahali hapo ilisababisha wao pia kusumbuliwa bila sababu.

“Kuna wakati fulani hata wakipiga doria katika eneo hilo wao hujaribu kutuhangaisha bure. Kwa hivyo, sisi kama kikundi cha Thingira Car Wash, tuliwasilisha matakwa yetu kwa mheshimiwa wetu Bw Wainaina,” alisema Bw Mucheru.

Mnamo Jumatano, mbunge huyo alizuru eneo hilo na kuwakabidhi sare hizo rasmi ili wajitambulishe kamili kama waoshaji wa magari.

“Nilisikia malalamishi yao na kwa haraka nikaonelea niingilie kati ili kikundi hicho kitambuliwe rasmi,” alisema Bw Wainaina.

Aliwahimiza wajiweke kwa vikundi ili waweze kufaidika na fedha za Maendeleo za CDF .

“Mimi nitakuwa tayari kusaidia vikundi ili viweze kupiga hatua. Kile sitafanya ni kutoa pesa kwa mtu binafsi,” alisema Bw Wainaina.

 

Alikihimiza kikundi hicho kuiga mfano wa wahudumu wa bodaboda wa Kiganjo ambao hivi majuzi baada ya kuungana wamezindua mradi wa kujenga jumba la ghorofa litakalowasaidia kwa biashara.

Alisema yeyote anayajihusisha na Siasa hawezi kufaidika na chochote huku akisema atahakikisha eneo lake la uwakilishi linatekeleza ajenda nne za serikali.

Aliwashauri wawe wakiweka akiba kila mara wanapokamilisha siku yao ya kazi.

Aliwashauri wawe na akiba yao halafu baadaye waende kwake kwa usaidizi huo.

“Nyinyi kama kikundi mkishajipanga nitakuwa tayari kuwapiga jeki na kuona ya kwamba mnapiga hatua katika biashara yenu,” alisema Bw Wainaina.

  • Tags

You can share this post!

Gwiji Kadenge kuzikwa nyumbani Vihiga

FAINALI AFCON: Je, Senegal itaweza kulipiza kisasi dhidi ya...

adminleo