• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
Wanachokisema baadhi ya wazazi kuhusu shule kufunguliwa

Wanachokisema baadhi ya wazazi kuhusu shule kufunguliwa

Na SAMMY WAWERU

MAONI tofauti yameendelea kutolewa kuhusu pendekezo la Wizara ya Elimu shule zifunguliwe mwezi Oktoba 2020.

Wadau katika sekta ya elimu wakiongozwa na Waziri, Prof George Magoha wanapendekeza shule zifunguliwe mnamo Oktoba 19.

Wizara ya Elimu tayari imeagiza walimu kurejelea shuleni Jumatatu, juma lijalo, ili kujiandaa kwa minajili ya kupokea wanafunzi.

Shule zote nchini pamoja na taasisi za elimu zilifungwa Machi 2020, baada ya Kenya kuthibitisha kuwa mwenyeji wa Homa ya virusi vya corona (Covid-19), kama miongoni mwa mikakati kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo ambao sasa ni janga la kimataifa.

Kufuatia pendekezo shule zifunguliwe mwezi Oktoba, baadhi ya wazazi wanahisi serikali haijaweka mikakati kabambe watoto warejee shuleni.

“Hatukatai watoto warudi shule, ila swali tunaloomba kujibiwa ni: Wamejenga madarasa ya kutosha ili kuafiki hitaji la umbali kati ya mwanafunzi na mwenzake?” amehoji Antony Kibui kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Kulingana na mzazi huyo wa watoto wawili wanaosomea kiungani mwa jiji la Nairobi, usalama wa wanafunzi dhidi ya virusi vya corona unapaswa kupewa kipau mbele, akihisi serikali haijaweka mikakati bora kuangazia suala hilo.

“Huenda wengi wetu tukakosa kurejesha watoto katika shule za kibinafsi, kwa sababu nyingi hazina uwezo baada ya kuyumbishwa na Covid-19. Shule za msingi msongamano wa wanafunzi umekuwepo tangu kitambo, shule zikifunguliwa idadi itakuwa vipi kwa kuwa wengi hawana uwezo wa gharama ya shule za kibinafsi? Serikali iweke mikakati maalum ya ufunguzi, ijenge madarasa ya kutosha,” akahimiza Bw Kibui.

Huku baadhi ya wazazi wakiridhia hatua ya Wizara ya Elimu, kuna wanaosema kwa sasa hawana pesa kurejesha watoto shuleni mwezi Oktoba.

“Mfano, wanangu wamenenepa muda ambao wamekuwa nyumbani na ina maana kuwa nitawanunulia sare zingine mpya. Biashara zimeathirika, kimsingi hatuna pesa kwa sasa na tunaomba serikali iratibu ufunguzi uwe Januari 2021,” amependekeza mzazi mwingine, kauli hiyo ikipigwa jeki na Antony Kabui.

“Kuna wazazi ambao wamelemewa na maisha ya mijini, wakapeleka watoto wao mashambani ili wajipange kikazi. Wengi walipoteza ajira kufuatia corona, chini ya wiki tatu tuambiane tu ukweli hawatamudu,” akaendelea kueleza.

Huku wazazi wakipendekeza ufunguzi wa shule uahirishwe hadi Januari, Katibu Mkuu wa Muungano wa kutetea walimu nchini (Knut), Wilson Sossion ameridhia pendekezo la Wizara ya Elimu, akisema watoto watakuwa salama wakiwa shuleni.

“Watoto watakuwa salama wakiwa shuleni ikilinganishwa na nyumbani, hata ikiwa changamoto hazitakosa,” Bw Sossion akasema akihimiza walimu kulinda wanafunzi shule zitakapofunguliwa.

  • Tags

You can share this post!

NASAHA: Jiandae kisaikolojia kukabiliana na halamba halumbe...

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia tumizi ya uakifishaji...