Habari Mseto

Wanachuo wasusia masomo mtandaoni

July 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na Reginah Kinogu

ZAIDI ya wanafunzi 5,000 wa Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi, Nyeri wamesusia kushiriki katika masomo kwa njia ya mtandao, wakidai taasisi hiyo haijagharimia huduma za intaneti ili kuwawezesha kufuatilia masomo hayo.

Wanafunzi hao ambao wamekuwa wakisoma kwa njia ya mtandao tangu Mei, walishikilia kuwa hawatarejelea masomo hayo hadi chuo kitakapofadhili huduma hizo.

Wakiongozwa na Katibu Mkuu, Bw Franklin Manyara, wanafunzi walisema muda wake wa matumizi uliisha kati ya Julai 10 na 19.

Hivyo, walisema watarejelea masomo yao tu wakati chuo kitawatumia data nyingine. “Tulitumiwa data kwa awamu kadhaa.

Muda wa matumizi wa data tulizotumiwa katika awamu ya kwanza uliisha Julai 10 huku muda wa zile tulizotumiwa kwenye awamu ya pili ukiisha Julai 19.Chuo kilikosa kututumia data nyingine Ijumaa,” akasema.

Chuo hicho kimekuwa kikiwanunulia wanafunzi data kuhakikisha kuwa wengi wanaendelea na masomo yao kama kawaida.

“Kama chama cha wanafunzi, tuliamua kuwaambia wanafunzi kususia masomo kwa wiki moja ili kukipa chuo muda kujitayarisha kununulia wanafunzi 4,500 data,” akasema.