Wanafunzi 3,000 kukosa fedha za elimu ya bure
Na WANDERI KAMAU
WANAFUNZI 3,000 hawatapata fedha za mgao wa serikali kulipia karo zao kwani shule wanazosomea hazijaweka majina yao katika Mfumo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Elimu ya Wanafunzi (NEMIS).
Fedha hizo ni za kulipia karo zao katika mpango wa elimu bila malipo katika shule za msingi na upili.
Katibu wa Elimu, Dkt Bellio Kipsang alisema hayo jana, akisema kwamba tayari serikali imetoa Sh33 bilioni kugharimia karo hizo.
Kulingana na katibu huyo, Sh30 bilioni zitatumika kuwalipia karo wanafunzi wa shule za upili huku Sh3 bilioni zikitumika katika Mpango wa Elimu ya Shule za Msingi Bila Malipo (FPE).
“Hatutatoa fedha zozote kulipia wanafunzi ambao hatuna majina yao. Sharti kuu ambalo limetolewa kwa shule zote ni kwamba lazima ziweke majina ya wanafunzi wao katika mfumo huo,” akasema Katibu.
Hii ni mara ya kwanza ambapo serikali inatumia mfumo huo, ikishikilia kuwa unazingatia uwazi kuhusu habari zote zinazomhusu mwanafunzi na shule anakosomea.
Mwaka uliopita, serikali ilitumia ripoti ambazo ziliwasilishwa kwake na walimu wakuu.
Wiki iliyopita, Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Upili (KESSHA) kilieleza malalamishi yake kwamba ucheleweshaji katika utoaji wa fedha hizo umeathiri sana baadhi ya shughuli kama ununuzi wa vifaa vya matumizi darasani.
Zaidi ya wanafunzi 700,000 walijiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.