• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Wanachuo watakiwa kuwa wabunifu baada ya masomo

Wanachuo watakiwa kuwa wabunifu baada ya masomo

Na LAWRENCE ONGARO

MBINU mwafaka ya wanafunzi kujitegemea kiuchumi baada ya kukamilisha masomo ya chuo kikuu ni kuwa wabunifu.

Haya ni kulingana na Naibu Chansela wa Chuo cha Jomo Kenyatta, (JKUAT), Juja, Profesa Victoria Ngumi.

Alisema Jumatano kuwa cha muhimu ni wanafunzi kutafuta ushauri wa kina kutoka kwa wasomi ili kuelewa jinsi ya kujiendeleza.

Alisema Chuo hicho kinazingatia maswala ya utafiti na ubunifu na kwa hivyo mwongozo huo ni tosha kumsukuma mwanafunzi katika kiwango kingine.

“Sisi katika chuo hiki tunawapa wanafunzi mwongozo ufaao wa jinsi ya kujisimamia wakati wowote wanapokamilisha masomo yao hapa. Kwa hivyo ni vyema kuonyesha ukakamavu unapotafuta ajira popote pale,” alisema Prof Ngumi.

Alitaja baadhi ya masomo yanayofunzwa hapo Chuoni kama Uhandisi, maswla ya Teknolojia ya ICT, Afya, ujenzi na utafiti kwa upande wa kilimo.

Aliyasema hayo katika kongamano ya siku tatu ya wanafunzi kuhusu jinsi ya kujitayarisha kwa kutafuta ajira baada ya kukamilisha masomo.

Meneja wa soko katika kampuni ya Bidco Africa Ltd Bw Chris Diaz, aliwahimiza wanafunzi hao kujiamini wanapotafuta ajira.

Aliwashauri wawe wabunifu ili kujitegemea badala ya kungoja ajira ambayo wakati mwingi huchukua muda kupata.

Alisema kampuni ya Bidco itafanya ushirikiano na Chuo cha Jomo Kenyatta (JKUAT), ili kuwaajiri wanafunzi kadha hasa wakati wanapokuwa likizo ili waweze kupata ujuzi zaidi jinsi ya kujitegemea baadaye.

Mhandisi wa kitengo cha uhandisi Benson Kariuki aliwataka wanafunzi wawe na uadilifu na nidhamu ili kufanikisha matakwa yao katika masomo.

“Bila kuwa na akili ya kujituma, kuwa na ubunifu na maadili mema bila shaka hata masomo yako yote hayatakuwa na thamana yoyote,” alisema Mhandisi Kariuki.

Alisema nchi hii inakosa kuwa na viwanda vingi kwa sababu ubunifu na maono hayajatiliwa maanani na wahusika.

Alitaja nchi za China, Japan Korea, na Canada kama zilizoendelea kwa sababu ya maono,ubunifu na mipangilio ya siku za baadaye.

You can share this post!

Sababu ya wanaume kuzeeka mapema kuliko wanawake

UG sasa kutumia wanawake warembo kuvutia watalii

adminleo