Habari Mseto

Wanafunzi wakerwa na chuo kutowapeleka mashindanoni

August 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEORGE NDISYA

WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Masinde Muliro wamekashifu kufutiliwa mbali kwa mipango ya kushiriki katika mashindano ya kitaifa ya muziki yanayoendelea Kabarak, Nakuru hata baada ya kujiandaa vilivyo.

Wamelaumu usimamizi wa chuo hicho kuwanyima nafasi hiyo kwa sababu ya madeni ya karo walio nayo.

Mwenyekiti wa kwaya ya chuo hicho, Bw Derick Shitambasi, alisema kuwa alitamaushwa sana na mabadiliko hayo yaliotekea dakika za mwisho za maandalizi ya washiriki.

“Usimamizi wa chuo unadai kuwa sababu za kufutilia mbali mpango wa kuwawezesha wanafunzi kushiriki mashindano hayo yanahusiana na madeni ya karo ambayo hayajalipwa,” akasema Bw Shitambasi.

Aliongeza kuwa safari ya wanafunzi hao ilikatizwa muda mfupi baada ya wao kujiandaa kusafiri.

Bw Sumba Shitambasi ambaye alihusika kwenye mipango ya safari hiyo alimtaka naibu chansela wa chuo Prof Asenath Sigot kuingilia swala hilo.

“Tuna imani kuwa chuo hiki kitabadili uamuzi wake na kuwapa wanakwaya nafasi ya kusafiri na kushiriki kwenye mashindano ya kitaifa kama ilivyokuwa imepangwa awali. Tayari tulikuwa tumejiandaa vilivyo,” akasema Bw Shitambasi.

Mashindano hayo yatamalizika Agosti 15.