Habari Mseto

Wanafunzi watundu watajua hawajui – Belio Kipsang

July 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na LUCY KILALO

SERIKALI imeshikilia msimamo wake mkali kuwa wanafunzi wanaojihusisha na migomo hasa uharibifu wa mali lazima waadhibiwe vikali.

Katibu wa Wizara ya Elimu, Dkt Belio Kipsang alisema hawataruhusu wanafunzi wachache kuvuruga shughuli za masomo.

“Hatutawaruhusu wanafunzi kuendesha shule zetu. Lazima wafuate miongozo ya wanaowasimamia,” Dkt Kipsang aliambia Kamati ya Elimu ya Bunge la Kitaifa inayoongozwa na mbunge wa Tinderet, Julius Melly.

“Hata wananchi huwa hawashauriwi kuhusu mabadiliko fulani yanapofanywa serikalini, na haitawezekana kwa wanafunzi kuanza kuamua ni nani ambaye atakuwa mkuu wa shule yao ama yale wanayotaka,” akasema.

Katibu huyo pia alisisitiza kwamba Serikali haitachangia kwa vyovyote katika urekebishaji wa mijengo iliyoharibiwa kwenye migomo, akisema wazazi wa wanafunzi waliohusika watabeba mzigo huo.

“Wazazi ambao watoto wao walishiriki katika kuharibu mali ya shule lazima wagharamie,” akadokeza.

Aliwataja wanafunzi wanaoongoza migomo na kuharibu mali ya shule kama wahalifu ambao hawataponyoka adhabu.

“Watapitia utaratibu unaostahili wa kisheria. Tayari kuna wanafunzi watatu wa shule ya Siakago ambao wamehukumiwa kifungo cha nje.

Pia alieleza kuwa polisi wangali wanawasaka wanafunzi waliowashambulia walimu katika shule ya Chalbi, Kaunti ya Marsabit.

Migomo ambayo imehusisha shule zaidi ya 40 sasa, iliibua mjadala katika kamati hiyo kuhusiana na wajibu wa wazazi na maadili, na iwapo kupigwa marufuku kwa kiboko kunachangia.

“Tulivyo sasa tunakalia bomu linalosubiri kulipuka. Tuliwacha pengo tulipoondoa kiboko,” alisema Mbunge wa Rangwe, Lilian Gogo.

Alieleza kuwa lazima taifa likiri kuwa kuna tatizo kubwa la wanafunzi hasa katika masuala ya maadili.