Wanahabari na mawakili waonywa dhidi ya kujadili kesi ya Monica
Na RICHARD MUNGUTI
MTANGAZAJI wa runinga Jacque Maribe na mchumba wake Joseph Irungu Jumatano walirudishwa rumande kwa siku saba zaidi huku familia ya marehemu Monica Nyawira Kimani ikiomba wasiachiliwe kwa dhamana kwa kuhofia maisha yao.
Katika ushahidi kwa mahakama uliowasilishwa na nduguye marehemu, Bw George Kimani anasema mshtakiwa wa kwanza Joseph Kuria Irungu, “ni hatari kwa usalama wa familia yao kwa vile haijajulikana sababu ya kuuawa kwa Monica.”
“Najua Irungu anajua ninakoishi. Nahofia maisha yangu ikiwa ataachiliwa kwa dhamana,” Bw Kimaai anasema katika afidaviti aliyowasilisha kortini.
Na wakati huo huo Jaji James Wakiaga anayesikiza kesi hiyo alivitahadharisha vyombo vya habari dhidi ya kuhujumu haki za washtakiwa kwa kuchapisha ushahidi ambao haujawasilishwa kortini.
“Nataka kuwatahadharisha wanahabari wote dhidi ya kuchapisha taarifa zozote za uchunguzi au mashahidi kuhusu kesi hii kabla haujawasilishwa kortini,” alisema Jaji Wakiaga.
Mbali na wanahabari pia aliwaonya mawakili dhidi ya kujadilia katika vyombo vya habari masuala yoyote kuhusu kesi hii dhidi ya Bi Maribe na mpenziwe Joseph Kuria Irungu almaarufu Jowi.
Jaji huyo alisema hataki kamwe kuchafuliwa mawazo yake na habari anazosoma kuhusu kesi hiyo anayoisikiza kabla ya ushahidi kuwasilishwa mbele yake.
“Nataka kuwakumbusha wanahabari kuwa sheria inayolinda haki za washukiwa ingalipo na watakaoikaidi basi watajilaumu wenyewe,” alitahadharisha Jaji Wakiaga.
Mawakili wanaowatetea washtakiwa pia walieleza kuighadhabika kwa nan a tabia ya wanahabari kuchapisha habari kuhusu kesi hiyo hata kabla ya ushahidi kuwasilishwa kortini.
“Tumeandika barua za kulalamika kwa baadhi ya wakuu wa vyombo vya habari dhidi ya kuchapisha ushahidi na taarifa nyingine za kupotosha ukweli kuwahusu washtakiwa,” alisema wakili Herman Omiti anayewakilisha Familia ya marehemu Monica Nyawira Kimani.
Jaji Wakiaga alitoa onyo hilo wakati wa kusikizwa kwa kesi ya mauaji inayaowakabili mwanahabari Maribe na mchumba wake Irungu.
Wote wamekanusha shtaka la kumuua mwanamke mfanyabiashara Monica Nyawira Kimani katika makazi yake mtaa wa Kilimani Nairobi.
Mawakili Katwa Kigen na Dunstan Omari wanaomtetea Bi Maribe na Mabw Samson Nyaberi na Cliff Ombeta walisema bado kiongozi wa mashtaka Bi Catherine Mwaniki hajajibu maombi ya washtakiwa ya kuachiliwa kwa dhamana.
“Bado Bi Mwaniki hajajibu maombi ya washtakiwa kuachiliwa kwa dhamana,” walisema Mabw Kigen na Nyaberi.
Pia Bw Omiti alisema bado mawakili hao wanaowatetea washtakiwa hawajajibu ombi la Familia ya mhasiriwa kupinga washtakiwa wakiachiliwa kwa dhamana.
Katika ombi la familia, mahakama imeombwa isithubutu kuwaachilia kwa dhamana washtakiwa ikidai “maisha ya baadhi yao iko hatarini ikitiliwa maanani jinsi Monica alivyouawa kinyama.”
Ushahidi uliowasilishwa kortini na nduguye marehemu Bw George Kimani unasema kuwa “ mauaji ya Monica ni ishara kuwa kuna uhasma uliofichika dhidi ya familia hiyo na haijulikani atakayeshambuliwa na mahasidi hawa wanaoendeleza vita vya kuviziana.”
Bw Kimani anasema kuwa uchunguzi wa kesi hiyo unaendelea na washtakiwa wakiachiliwa kwa dhamana watavuruga shughuli hiyo sawia na kuwatisha mashahidi waliorodheshwa kutoka kwa familia ya marehemu kufika kortini kueleza wanachojua.
“Bado haijajulikana sababu na kiini cha kuuawa kwa Monica na endapo washtakiwa wataachiliwa huenda wakaendeleza msururu wa mauaji,” anasema Bw Kimani.
Jaji Wakiaga aliamuru washtakiwa wasalie ndani hadi Oktoba 24 wakati atakaposikiza ombi lao la dhamana.
Pia aliamuru idara ya urekebishaji tabia iwasilishe ripoti kuwahusu washtakiwa kabla ya kuamuwa ikiwa atawaachilie kwa dhamana au la.
Bali na hayo, Jaji Wakiaga aliamuru Irungu apelekwe hospitali kuu ya Kenyatta (KNH) kufanyiwa upasuaji mkono uliopigwa risasi.