• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 5:45 AM
Wanaharakati waelezea mbinu mbadala za kukabiliana na Al Shabaab

Wanaharakati waelezea mbinu mbadala za kukabiliana na Al Shabaab

NA KALUME KAZUNGU

WANAHARAKATI wa uhifadhi wa mazingira Kaunti ya Lamu wanaitaka serikali kubuni kambi za kudumu za maafisa wa huduma kwa wanyama pori (KWS) na wale wa uhifadhi wa misitu (KFS) ndani ya msitu wa Boni kama njia mojawapo itakayoleta suluhu kwa tatizo la usalama eneo hilo.

Msitu wa Boni umekuwa ukitumiwa na magaidi wa Al-Shabaab kama ngome yao ya kujificha kila wakati wanapotekeleza mashambuklizi na mauaji kwenye kaunti za Lamu, Garissa na Tana River.

Mnamo Septemba, 2015, serikali ilianzisha operesheni kwa jina Linda Boni yenye lengo la kuwafurusha Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani yam situ huo.

Wakizungumza na wanahabari mjini Lamu aidha, wanaharakati hao wa uhifadhi wa mazingira walisema iwapo serikali itabuni kambi za kutosha za KWS, KFS na hata mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali na ambayo hushughulikia uhifadhi wa mazingira, huenda hali hiyo ikachangia Al-Shabaab kuutoroka msitu huo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uhifadhi wa Mazingira na Wanyama Pori Kaunti ya Lamu, Ali Shebwana, anasema haoni haja ya serikali kuendelea kutumia mabilioni ya fedha katika kupigana na Al-Shabaab ndani yam situ wa Boni.

Badala yake, Bw Shebwana aliitaka serikali kuibuka na mbinu mbadala, ikiwemo ile ya kuanzisha shughuli mbalimbali ndani yam situ huo ambazo zitawanyima Al-Shabaab mahali pa kujificha.

Alisema huenda Al-Shabaab wamepata mwanya wa kujificha ndani ya msitu wa Boni kutokana na kwamba sehemu nyingi za msitu huo zimetelekezwa hasa kishughuli.

“Ni bayana kwamba serikali haiwezi kumaliza Al-Shabaab kwa kusambaza polisi na wanajeshi wengi kupiga doria kwenye msitu wa Boni.

Ningeomba serikali badala ya kuendelea kutumia mabilioni ya fedha kwa operesheni, fedha hizo zitumiwe kuanzisha kambi za KWS, KFS na shughuli nyingine nyingi ndani ya msitu huo. Msitu wa Boni uko na wanyama wengi na miti ya kila aina. Unaweza kutumika kama kivutio cha watalii.

Ikiwa hilo litafanyika basi huenda Al-Shabaab wakose pa kujificha na wahame kwenye msitu huo,” akasema Bw Shebwana.

Afisa huyo aidha alipinga vikali pendekezo la serikali la kutaka kuulipua msitu wa Boni kama njia mojawapo ya kumaliza Al-Shabaab.

“Huu msitu umekuwa ukitumika na jamii yenyewe ya Waboni ili kuendeleza shughuili zao za uchumi, ikiwemo kuwinda wanyama pori, kuvuna asali ya mwituni na kuchuma matunda. Kuulipua msitu ni sawa na kuharibu rasilimali ambayo serikali imechukua muda mwingi kuihifadhi,” akasema Bw Shebwana.

  • Tags

You can share this post!

Ombeta alalamikia masharti makali ya dhamana kwa wateja wake

Boya lililotoweka baharini lasakwa

adminleo