• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 5:45 AM
Wanakijiji wawaka wakidai chifu mpenda hongo alisababisha kifo cha muuzaji chang’aa

Wanakijiji wawaka wakidai chifu mpenda hongo alisababisha kifo cha muuzaji chang’aa

NA STEVE MOKAYA

Jumanne, mwendo wa saa kumi na moja jioni, Wilfred Omoyo Nyaanga, mwenye umri wa miaka 47, na baba wa mtoto mmoja wa kiume alifariki katika mazingira tatanishi.

Marehemu, ambaye alikuwa muuzaji wa pombe haramu, alifia nyumbani kwake, katika kijiji cha Gechona, lokesheni ya Miriri, katika kaunti ndogo ya Masaba Kaskazini, Kaunti ya Nyamira.

Wanakijiji na jamaa ya mwenda zake, ambao walikuwa wamejaa hasira, walikataa polisi kutoka kituo cha Keroka kuchukua maiti yake.

Kisa na maana, ni kuwa walitaka Chifu wa eneo hilo, Naftal Ongaki, awasili katika eneo la mkasa na kujibu maswali yao kabla ya maiti kuchukuliwa. Ila, chifu huyo hakuenda kwa kuhofia usalama wake, na hivyo polisi walirudi kituoni na gari lao, pasi na maiti waliyokujia.

Chifu Naftal Ongaki. Picha/ Steve Mokaya

Hata hivyo, Jumatano saa tano asubuhi, maafisa kutoka kituo cha polisi cha Keroka, waliwasili, na kuchukua maiti, baada ya maongezi na wanakijiji na jamii.

“Hatukutaka kutumia nguvu, jana kuchukua maiti, kwa sababu watu walikuwa wamekasirika, na pia walikuwa wanaomboleza. Na iwapo tungetumia nguvu, watu hao hao ndio wangeumia, na hatukutaka hilo litendeke,” alisema askari mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe, kwa vile hana ruhusa ya kutoa semi rasmi.

Wanakiji wanamlaumu chifu na manaibu wake kwa kusababisha kifo cha mzee Wilfred Omoyo Nyaanga.

Hata hivyo, Naibu chifu wa Lokesheni ndogo ya Miriri, Elijah Nyaenya, ambaye alikuwa kwenye eneo la mkasa kabla ya mauti hayo kutokea, aliongea na Taifa Leo Dijitali na kukanusha madai kuwa wao ndio chanzo cha kifo cha marehemu.

Mwili wa mwendazake ukipelekwa katika gari la polisi. Picha/ Steve Mokaya

“Jana tulipata habari kuwa marehemu ameonekana na wananchi akiwa na vibuyu vya chang’aa. Chifu akanituma niende na wazee wa kijiji na kuchukua pombe hiyo. Hivyo, nilienda na wazee wawili ambao ni Peter Momanyi na Mokaya Ngoko.

“Wawili hao walinitangulia kwa dakika chache. Nilipofika, nikapata mwendazake amezirai. Tulichukua pombe hiyo kwenye vibuyu viwili na simu yake tukaja nayo ofisini. Alipozirai, niliwaambia ndugu zake wamfanyie huduma ya kwanza, ila nilipofika ofisini, nikasikia kuwa ameaga dunia,” anasema naibu Chifu, Elijah Nyaenya.

Hata hivyo, wanakijiji nao wanadai kuwa wazee hao walioandamana na naibu chifu ndio walimpiga marehemu baada ya kukataa kuwapa pesa. Wanadai kuwa ni kutokana na kipigo hicho ambapo aliiaga dunia.

Wakazi waliojawa na hamaki walidai chifu huyo alisababisha kifo cha mwenazake kwa mazoea yake ya kumwitisha hongo. Picha/ Steve Mokaya

Kulingana na James Kiyaka, ambaye ni binamu ya marehemu, mwendazake alikufa kwa kupigwa.

“Walikuja na kumwomba pesa ambazo chifu amezoea kumwomba ili amkubalie auze pombe yake. Alipowakataza, wakaanza kumpiga, akaanguka chini na kuzirai, na akafa baadaye,” anasema Kiyaka.

Hata hivyo, Mokaya Ngoko, ambaye ni mmoja wa wazee walioandamana na naibu chifu, alikana madai ya kumpiga.

“Sisi tulifika tukampata akiwa ameketi chini kwenye nyumba yake, mlevi. Alipotuona, akakunywa pombe iliyokuwa kwenye jagi, na ingine akatumwagia. Baadaye alianguka na kuzirai. Wala hatukumpiga,” anasema.

Samuel Omoyo, ambaye ni mtoto wa pekee wa marehemu, na mwanafunzi wa darasa la nane alisema, “Nilikuwa kwenye kinyozi nilipopigiwa simu na kuambiwa kuwa baba ni mgonjwa. Nikachukua muda mfupi kufika nyumbani. Nilipowasili kwenye nyumba, nilipata baba akiwa amelala chini, akiwa mfu,” anasema.

Hatimaye, mwili uliondolewa Jumatano. Picha/ Steve Mokaya

Samuel alisema kuwa asubuhi hiyo, walikuwa wameongea na babaye, naye akamwambia kuwa alikuwa anaenda kutoa shilingi elfu hamsini kutoka kwenye akaunti ili afanyie biashara, ili kuzidisha pesa zitakazompeleka shule ya upili mwaka ujao.

“Nadhani kuwa wakati naibu chifu alikuja, baba alikuwa na hizo pesa, na huenda walizichukua; kwa sababu pia walichukua simu yake,” anasema.

Fauka ya hayo, Samuel anasema kuwa ilikuwa ni kawaida ya chifu kukusanya pesa kati ya elfu moja na elfu tatu kutoka kwa babake kila mwezi, ili amkubalie kuendesha biashara yake ya kuuza pombe.

Hata hivyo, Chifu Naftal Ongaki alikana madai hayo.

“Mimi hata huwa siendi huko. Hata sikuwa najua kuwa anauza pombe. Mimi nilipewa tu habari na wananchi kuwa fulani ameonekana na pombe haramu, nami nikamtuma naibu wangu akalete pombe hiyo ofisini,” anasema.

Chifu alisema kuwa hayo ni madai ambayo yanalenga kumharibia sifa na kumfanya alegeze vita dhidi ya pombe haramu, ila akasema kuwa vita hiyo bado itaendelea.

Wanakijiji wakiongozwa na Sam Omwamba Mobunde, waliiomba serikali kuingilia kati na kukomesha visa vya ufisadi kati ya viongozi wa serikali na wananchi, na pia kukomesha biashara ya chang’aa kijijini.

“Tunamwomba waziri Matiang’i atusaidie. Machifu wake na viongozi wa serikali huku wameoza. Huyu aliyekufa ni mtu wa saba kwa sababu ya chang’aa. Kama hawatafanya jambo, tutachukua sheria mkononi,” alisema.

Naibu kamishana wa kaunti ndogo ya Masaba Kaskazini, Benson Leparmojo, alikiri kujua kifo cha marehemyu, ila akasema kuwa uchunguzi utafanywa ili kuweka wazi chanzo cha maiti yake.

“Eneo hilo ambako kisa hicho kilitokea liko na historia ya ukosefu wa nidhamu na usalama. Hata ndio maana maafisa wetu wa usalama hawakutumia nguvu kuchukua maiti siku ya Jumanne jioni. Chang’aa imeharibu maisha ya watu wengi. Hata hivyo, tuna mipango ya kuweka kituo cha polisi katika eneo hilo ili kupunguza uvunjaji wa sheria na kuleta usalama,” anasema.

Fauka ya hayo, alisema kuwa baada ya uchunguzi kutamatika, yeyote atakayepatikana na makosa, hata kama na chifu ama manaibu wake, sheria itachukua mkondo wake. Alisema kuwa matokeo ya uchunguzi yatawekwa wazi mapema iwezekenavyo.

Mwili wa mwendazke ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Keroka.

You can share this post!

MAUAJI YA MTANGAZAJI: Mwanamume mwenye umri wa miaka 23...

Mwanamke jela mwaka mmoja kwa kujaribu kumuua mtoto

adminleo