Wananchi kuumia zaidi bei ya mafuta ikipanda
Na WANDERI KAMAU
SIKU moja baada ya bajeti kusomwa, Wakenya wameanza kuhisi athari zake huku Mamlaka ya Kudhibiti Kawi (EPRA) ikiongeza bei za mafuta.
Kwenye tangazo lililotolewa Ijumaa, bei ya petroli ilipanda kwa Sh3.07 kutoka Sh112.63.
Bei ya dizeli pia ilipanda kwa senti 0.39 kutoka bei ya sasa ya Sh104.37.
Hata hivyo, bei ya mafuta taa ilipungua kwa senti 0.4
Jijini Mombasa, petroli itauzwa kwa Sh112.45, dizeli Sh102.13 huku mafuta taa yakiuzwa kwa Sh101.65. Jijini Kisumu, petroli itauzwa kwa Sh116.56, dizeli Sh106.45 na mafuta taa kwa Sh105.97.
Tangazo hilo linamaanisha kuwa gharama ya maisha itazidi kupanda, hasa shughuli za usafiri na bei za bidhaa za kimsingi kuathirika.
Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Bw Pavel Oimeke, alihusisha hali hiyo na ongezeko la bei ya mafuta ambayo hayajasafishwa katika soko la kimataifa.
Akitoa taarifa yake kwa Kamati ya Seneti kuhusu Kawi mnamo Jumatano, mkurugenzi huyo alisema bei hizo zimeongezeka kutokana na gharama za juu za usafirishaji, kodi na usambazaji wake.
“Gharama ya mafuta ghafi katika soko la kimataifa huchangia sana katika uamuzi wa bei za mwisho nchini. Kwa muda wa miezi mitano iliyopita, bei ya mafuta ghafi imekuwa ikiongezeka katika soko la kimataifa, hali ambayo imetulazimu kuwianisha bei zetu na hali ilivyo,” akasema.
Mkurugenzi huyo alikuwa amealikwa na kamati hiyo kueleza sababu za kuongezeka kwa bei za mafuta katika miezi ya hivi karibuni, hali ambayo imechangia kuongezeka kwa gharama ya maisha.
Tangazo hilo linaonekana kukinzana na kauli ya serikali, kuwa lengo kuu la bajeti ya mwaka 2019/2020 iliyosomwa Alhamisi, ni kupunguza gharama ya maisha kwa mwananchi.