• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Wanaodaiwa kuua binti wa hakimu kujibu mashtaka Ijumaa

Wanaodaiwa kuua binti wa hakimu kujibu mashtaka Ijumaa

Na Alex Njeru

WASHUKIWA wawili wa mauaji ya binti wa hakimu wa mahakama ya Githongo, Meru Jumatatu walikosa kusomewa mashtaka kwa mara ya pili baada ya Mahakama Kuu mjini Chuka kukataa ripoti ya uchunguzi wa akili ikisema ilikuwa na makosa.

Jaji Robert Limo alisema ripoti hiyo iliyotayarishwa na hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Meru mnamo Oktoba 4, 2018, haikueleza ikiwa ni serikali au washukiwa Benson Kimathi Marangu na Francis Otudo waliochunguzwa.

“Jinsi ripoti hii imeandikwa, siwezi kusema inataja nani kati ya serikali na washukiwa,” alisema Jaji Limo.

Kiongozi wa mashtaka, Bi Jane Maari alikubali kwamba ripoti hiyo ya matibabu ilikuwa na makosa na akaomba wiki mbili ili irekebishwe.

Hata hivyo, Jaji Limo alisema washukiwa wana haki ya kushtakiwa haraka iwezekanavyo. Alisema kesi hiyo inafuatiliwa na umma na haifai kucheleweshwa.

Jaji Limo aliagiza upande wa mashtaka kuwasilisha ripoti inayotaja majina ya washukiwa ili wasomewe mashtaka Novemba 2.

Jaji Limo pia alikubali ombi la wakili wa Bw Marangu, Bw Elias Mutuma, kuwasilisha ombi la kuachiliwa kwa dhamana tarehe hiyo. Kesi hiyo ilihamishwa kutoka Mahakama Kuu ya Meru kwa sababu marehemu ni binti yake Carol Kemei, Hakimu wa mahakama ya Githongo, ambayo iko chini ya Mahakama Kuu ya Meru.

Bw Marangu alikuwa askari wa gereza la Kangeta. Msichana Maribel

Kapolon alitekwa nyara Septemba 6 na mwili wake kupatikana katika msitu wa Gitoro siku 11 baadaye.

Ripoti ya mwanapatholojia ilionyesha kuwa alikufa kutokana na majeraha ya kupigwa kichwani mara kadhaa.

  • Tags

You can share this post!

Savula na wake zake wakana kumumunya mamilioni ya serikali

Polisi auawa na wanakijiji baada ya kumuua mkewe

adminleo