Habari Mseto

Wanaoendesha bodaboda bila leseni waonywa

July 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MISHI GONGO

AFISA wa trafiki eneo la Pwani Bw Peter Kimani amewaonya vijana wasio na ujuzi kuendesha pikipiki barabarani akisema kuwa watu hao ndio wanachangia kuongezeka kwa ajali.

Alisema Alhamisi kwamba vijana wengi wanaoendesha bodaboda mjini Mombasa hujifunza kutoka kwa rafiki zao ikimaanisha kwamba wanakosa ufahamu wa baadhi ya sheria, kanuni na alama za trafiki.

“Unapofundishwa kupeleka pikipiki mitaani, unajikosesha nafasi ya kufundishwa sheria na kanuni za barabarani hivyo kujiweka katika hatari ya kusababisha ajali,” Bw Kimani akasema.

Kamanda huyo alisema tangu kufungwa kwa shule ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona, vijana wa shule wamekuwa katika maegesho ya pikipiki wakijifunza biashara hiyo.

“Baada ya kijana kujihisi amejua kupeleka pikipiki, anaazima pikipiki na kuruhusiwa kubeba abiria. Hatua hii inahatarisha maisha ya abiria na anaeendesha pia,” akasema.

Alisema watu hawa ndio huonekana wakipisha magari kwa upande usio sahihi.

Alionya kuwa watafanya msako wa kuwatoa wanaofanya biashara ya bodaboda bila leseni.

Bw Kimani aliwahimiza walio na nia ya kufanya biashara hiyo kujisajili kwa kufuata sheria hitajika.

Aidha aliwashauri wahudumu hao kujichukulia leseni na kukata bima ya kuwalinda iwapo watahusika katika ajali.

Wakati huo huo, aliwasisitiza wahudumu wote kufuata masharti yaliyowekwa na Wizara ya Afya ili kujikinga kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Aliwahimiza kubeba abiria mmoja kwa kila safari ili kuweza kuekeana umbali kama walivyoagizwa na wizara.