• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Wanaohusudu tohara ni wapumbavu, Raila asema

Wanaohusudu tohara ni wapumbavu, Raila asema

NA WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, amewakashifu vikali watu ambao wamekua wakitumia tohara kama kipimo cha uwezo wa uongozi bora, akiwataja kuwa “wapumbavu”.

Akihutubu Jumatatu katika eneo la Teso Kaskazini kwenye mkutano na viongozi wa chama cha ODM katika eneo hilo, Bw Odinga alitaja tohara kama tamaduni ya kigeni “iliyoletwa Afrika kwa njia ya dini”.

“Tamaduni hii ya tohara huwa inaendeshwa tu na jamii za Kibantu kutoka Kenya. Ni jambo lisilo na maana lililokuja pamoja na dini. Lililetwa Kenya kwa jamii za Kibantu kupitia dini. Jamii za Kibantu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) huwa haziwatahiri wanaume wake. Hali ni kama hiyo nchini Afrika Kusini na Cameroon. Yeyote anayeichukulia tamaduni hiyo kwa uzito ni mpumbavu,” akasema Bw Odinga.

Kauli ya Bw Odinga ilionekana kuwalenga baadhi ya viongozi, ambao wamekuwa wakieneza dhana kuwa baadhi ya jamii hazifai kushikilia nafasi muhimu za uongozi na kisiasa nchini, kwani huwa haziwatahuri wanaume wake.

Dhana hiyo imekuwa ikienezwa hasa katika nyakati za uchaguzi.

Baadhi ya viongozi ambao washawahi kujipata matatani kwa kueneza dhana hiyo ni Waziri wa Utumishi wa Umma, Moses Kuria.

Kwenye kesi iliyowasilishwa mahakamani na Tume ya Kitaifa ya Utangamano na Mshikamano (NCIC) mnamo 2020 dhidi yake, Bw Kuria alishtakiwa kwa kuiharibia jina jamii moja, akidai kwamba haifai kuchukua nyadhifa zozote za uongozi kwa kutowatahiri wanaume wake.

Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa Bw Kuria kufunguliwa mashtaka kama hayo, baada ya kukabiliwa na mashtaka mengine mnamo 2015.

Mnamo 2008, dhana hiyo pia ilitajwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Hague, Uholanzi, kuwa miongoni mwa sababu zilizochangia ghasia za kikabila zilizotokea nchini baada ya uchaguzi tata wa 2007.

  • Tags

You can share this post!

Athari za El Nino Mukuru-Kayaba

Ubora wa mbegu za kiume hushushwa na hewa chafu

T L