• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Wanaopuuza onyo la mafuriko kuhamishwa kwa lazima

Wanaopuuza onyo la mafuriko kuhamishwa kwa lazima

STEPHEN ODUOR Na BRIAN OCHARO

SERIKALI imeonya kwamba wakulima katika Kaunti ya Tana River ambao wanakaidi ushauri wa mafuriko, wataondolewa kwa nguvu kutoka katika vijiji vilivyo na hatari ya mafuriko.

Kamishna wa Kaunti ya Tana River, David Koskei, alisema serikali imeongeza wito kwa watu walio hatarini kurejea kambini lakini baadhi wanashikilia kuendelea kulima na kuvuna mazao yao.

“Mto tayari umefurika na unaingia mashambani, bado mtu anakaidi. Hilo halitaruhusiwa,” alisema.

Bw Koskei alisema ingawa inaumiza kuona mimea ikizama karibu na hatua ya mavuno, maisha ni muhimu sana na yatalindwa kwa gharama yoyote.

Alitoa wito kwa wakulima ambao bado wapo kwenye mashamba yao kurejea kambini kabla ya hali kuwa mbaya.

“Kuweka maisha yako hatarini ni kosa la kihalifu, na serikali iko wazi kabisa na imetoa onyo mara kadhaa, tuwe watiifu,” alisema.

Mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa kufikia sasa yamekatiza barabara za Tana River na Garissa na kusababisha shida ya usafiri na hasara ya mamilioni ya pesa kwa madereva wanaosafirisha mazao.

Kulingana na Afisa Mkuu wa Mipango Maalum katika kaunti, Bi Salma Makuru, hali hiyo huenda ikasababisha kupanda kwa bei ya vyakula siku chache zijazo.

Bi Makuru anabainisha kuwa vijiji zaidi ya 11 kwa sasa vinaingiwa na maji kutoka kwa Mto Tana, hivyo basi Bwawa la Masinga likianza kumwaga maji hali itakuwa mbaya zaidi.

Alisema zaidi ya familia 25,000 kwa sasa ziko kambini na msaada wa dharura unahitajika.

Kwingineko Mombasa, sehemu ya barabara ya Links katika mtaa wa Nyali ilikuwa bado haipitiki kwa siku ya nne mnamo Jumamosi.

Mamlaka ya Barabara za Mijini Kenya (Kura), ilitoa tahadhari kwa madereva kutafuta njia mbadala.

Barabara nyingine kadhaa za Kisauni na ndani ya jiji pia zilijaa maji baada ya mvua kubwa kunyesha asubuhi lakini maji hayo ya mafuriko yalipungua ndani ya saa chache.

Maafisa wa Kaunti ya Mombasa walijitahidi kuzibua mabomba ya maji hasa katikati ya jiji.

  • Tags

You can share this post!

Afueni yaja Machogu akizitaka shule kupunguza karo

‘Ufisadi wa polisi, kanjo utaponza Thika kuwa jiji’

T L