Habari Mseto

Wanasiasa wa South Rift sasa wamtetea Koros

March 5th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

MATATIZO yanayokumba Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) yamechukua mkondo wa kikabila baada ya viongozi wa kisiasa kutoka eneo la South Rift kujitokeza kumtetea Afisa Mkuu Mtendaji wa hospitali hiyo, Bi Lily Koros.

Wakiongozwa na Gavana wa Kericho, Prof Paul Chepkwony, viongozi hao jana walikosoa hatua ya Waziri wa Afya, Bi Sicily Kariuki, kumpa Bi Koros likizo ya lazima baada ya mgonjwa kufanyiwa upasuaji wa kichwa kimakosa hospitalini humo wiki iliyopita.

“Baada ya kushauriana tumebaini kama viongozi wa Kaunti ya Kericho kwamba kuna juhudi zinazoendelezwa na watu fulani iwe wako serikalini, katika siasa au makundi ya watu binafsi wanaolenga kuondoa watu wa jamii moja mamlakani na kuweka watu ambao wanawapendelea,” akasema kwenye kikao cha wanahabari Nairobi.

Bi Koros aliagizwa kuenda likizo ya lazima pamoja na naibu wake, Dkt Bernard Githae, Ijumaa ili kutoa nafasi uchunguzi ufanywe kuhusu kisa hicho cha Jumatatu iliyopita.

Visa vingine vilivyofanya hospitali hiyo igonge vichwa vya habari mwaka huu ni wizi wa mtoto na madai ya ubakaji wa kina mama waliojifungua.

Prof Chepkwony alisema madai ya ubakaji yalibainika kuwa ya uongo huku wizi wa mtoto ukitatuliwa na mshukiwa kufikishwa mahakamani na hivyo basi akahisi kuna nia fiche kuhusu uamuzi wa kumwadhibu Bi Koros.

“Haieleweki jinsi anahusishwa na masuala ya upasuaji. Kuna wataalamu waliofunzwa wenye ufahamu kuhusu mambo haya na ambao wanafaa kuwajibika moja kwa moja,” akasema Chepkwony.

Mnamo Jumamosi, wabunge kutoka Kaunti ya Kericho wakiongozwa na Seneta Aron Cheruiyot, walidai kuna njama ya kumsimamisha kazi Bi Koros kwa sababu ana misimamo mikali ya kuzuia ufujaji wa pesa za umma katika hospitali hiyo.

Kulingana naye, KNH ni miongoni mwa taasisi za serikali ambazo zinatarajiwa kutengewa kiasi kikubwa cha pesa ili kufanikisha malengo ya serikali ya Jubilee kuhusu utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wote.

Hata hivyo, hatua ya viongozi wa kisiasa kujitokeza kutetea watu wa makabila yao wanaojikuta katika hali kama hii hata kabla uchunguzi kukamilika si jambo geni humu nchini.