Wanasiasa wachochezi kukabiliwa vikali
Na RUTH MBULA
WIZARA ya Usalama wa Ndani inabuni kanuni itakayohakikisha kuwa taifa halitatumbukia kwenye ghasia jinsi ilivyoshuhudiwa awali nyakati za uchaguzi.
Katibu wa wizara hiyo Karanja Kibicho alisema Jumatano kuwa watu wanaoeneza chuki watakabiliwa vikali kwani ndio kiini cha migawanyiko ya kisiasa nchini.
Bw Kibicho alizungumza katika mkutano na viongozi wa Kaunti ya Kisii kabla ya kuanza ziara yake ya ukaguzi, huku kaunti hiyo ikijitayarisha kuandaa sherehe za Sikukuu ya Mashujaa hapo Oktoba 20.
Huku akipuuzilia mbali nembo ya ‘deep state’, katibu huyo alisema hakuna aina yoyote ya ‘matusi’ itakayozuia azma yake ya kuwahudumia Wakenya.
“Tutahakikisha kuwa tunaendelea kutoa huduma kwa raia ikiwemo kupiga vita Alshabaab na pombe haramu pamoja na aina nyingine za uhalifu. Ninasisitiza kwamba hatutatishiwa na yeyote ili tukae kimya. Hatutaingizwa uwoga wala hatutalegeza kamba kamwe,” alisema akieleza kuwa wataendelea kufanya jinsi walivyoagizwa na Rais Uhuru Kenyatta ili kuhakikisha kwamba usalama umedumishwa nchini.
Alisema kuwa Huduma Namba haikuwa mzaha na kwamba ilikuwa miongoni mwa miradi mingi ambayo ni sharti watekeleze kwa hisani ya uongozi wa Rais Kenyatta.
Katibu huyo alisema wanatazama na hawatajaribu kutofautisha kati ya watu wanaoonekana kama wapole au wasio wapole mradi tu wanatoa hotuba zitakazosababisha vurumai nchini.